Wednesday, October 31, 2012

Vijana mkiamua



WINGI wenu twaujua, ndio wengi Tanzania,
Kura mkisajiliwa, nchi hii mwachukua,
Wakati umewadia, ajizi ni kuchelewa,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Mwtakiwa chini kaa, mikakati  kuizua,
Wengine mkiachia, mambo yenu kufulia,
Mida inshafikia, nchi yenu kuchukua,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Tena kwa demokrasia, bila nguvu kutumia,
Wajao kuwanunua, ya kwao kuitikia,
Mshiko kuuchukua, wengine mkachagua,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Chungueni yao nia, uzuri nauhofia,
Naamini wana mbaya, kitu wamedhamiria,
Utumwani kuwatia, vyao mkishajilia,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Ni mabwege mtakuwa, nafasi kutowaachia,
Mabavu wakatumia, nchi kujiongozea,
Ikawa kwetu balaa, kama ya Yugoslavia,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Hamsini wanafaa, umri walofikia,
Viongozi wenu kuwa, si zaidi kuzidia,
Akili zao ruia, bora hawataamua,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Ukubwa wanaunywea, na kokeni kuvutia,
Makubwa waazimia, hadi nchi kununua,
Mkenge mkiingia, watu wote twapotea,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Mirija yatapakaa, fukara kuwanyonyea,
Kisha zikazungushiwa, mikononi kurejea,
Kama vile wanapewa, chao wasichokijua,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Kila nikifikiria, nataka muweke nia,
Wengine kutowazuzua, wenyewe kujisimamia,
Ukubwa mmeingia, na sasa ni kuamua,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Makubwa kuyaamua, sasa kazi inakuwa,
Kwanza kuyafikiria, na kisha kujipimia,
Haki linalochukua, hilo kutolikataa,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Uwazi kuutumia, vyanzo vyote kuvijua,
Na nia ya wagombea, na waliowanunua,
Na nini wakusudia, nchi hii kufanzia,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Tarehe mkazitia, mambo kuyaangalia,
Na kama yasipotimia, kofia mkazivua,
Mkiipenda Tanzania, ni kisafi kuchagua,
Vijana mkiamua, nchi bora mtapata.

Mola ninawaombea, apate wabarikia,
Kweli mkiiamua, vingine haitakuwa,
Ni yenu demokrasia, budi kwenu kutumia,


No comments: