Wednesday, October 31, 2012

KUTONUNULIWA




Wahariri mashujaa, nienzio Tanzania,
Nyaronyo namkumbatia, siwezi nikamuachia,
Mkataa kununuliwa, ni mhariri shujaa,
Wahariri ushujaa, nyie kutonunuliwa !

Wasiokuwa na njaa, vya watu wakababia,
Rahisi kununuliwa, wachovu kuwanunua,
Dhuluma wakailea, kiyama kuyajutia,
Wahariri ushujaa, nyie kutonunuliwa !

Dini sintoangalia, kote wananunuliwa,
Roho naiangalia, wito inayoitikia,
Haki kuisimamia, si shetani kumfaa,
Wahariri ushujaa, nyie kutonunuliwa !

Hawa kwangu ni shujaa, kwa nyingi huba na hawa,
Ninawapenda radhia, na heshima naitia,
Lao nitalisikia, na yao kujisomea,
Wahariri ushujaa, nyie kutonunuliwa !

Waongo waliokuwa, bwana kutumikia,
Kama mbwa kuja kuwa,  ovyo wanajibwekea,
Hao kwangu udhia, hata kama nawazaa,
Wahariri ushujaa, nyie kutonunuliwa !

Kwangu kina malkia, ukweli wanaujua,
Haki wanaitetea, na wanyonge kuwafaa,
Ila wanaotumiwa, kwangu mimi changudoa,
Wahariri ushujaa, nyie kutonunuliwa !

Fakiri ninajijua, wapi pakusimamia,
Kesho nimeshachagua, leo ninaiachia,
Wangu wanaonifaa,njia yangu kufatia,
Wahariri ushujaa, nyie kutonunuliwa !

Njiani wanaorudia, kuritadi wafanzia,
Siwezi wavumilia, wala kuwaangalia,
Nahesabu mfu wawa, kitu hawatatufaa,
Wahariri ushujaa, nyie kutonunuliwa !

No comments: