Wednesday, October 31, 2012

Isiwe adui wewe




Katika hii miaka, huwa usiyemdhania,
Nafusi kughalifika, mwingine kumdhania,
Na wajanja wazaliwa, hili wanalitumia,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Chako atakuibia, yule akasingiziwa,
Yule ukimvamia, yeye anajichimbia,
Pupa ukiitumia, pabaya wenda ingia,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Vyama vitakuambia, udini huyo kajaa,
Ukiivuta pazia, kumbe ndio walokuwa,
Yanapokuja tokea, mwengine asingiziwa,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Wamezuka wa kuzua, waitwa mapakazia,
Uchuro wanautia, kuiharibu dunia,
Uoza kuusifia, na maradhi kuutia,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Watu wananunuliwa, wengine kuwasingizia,
Imani wasiokuwa, mbwa mwitu wa dunia,
Kazi yao kutumiwa, makombo wakaachiwa,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Njaa yao inachipua, hadi kuwa ukichaa,
Kitu kutofikiria, mitegoni huingia,
Jema wakliachia, uovu kuununua,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Watu wa kusingizia, na uongo kuufua,
Pasi kisha kuutia, mvaa akajivalia,
Zama zinawaachia, giza likajitandia,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Wakubwa watatumia, waliokonda kwa njaa,
Dhima wakaichukua, wamiliki nao kuwa,
Na hicho wanachopewa, ni hadithi nakwambia,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Kinamama huugua, uzuri kukimbilia,
Nje wakiangalia, dhahabu wakadhania,
Ndani wangeliujua, hilo wasingekaribia,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Huchekwa lile la kulia, la kucheka wakalia,
Ilivyoota hadaa, na zaini kuchanua,
Ukiyaona maua, sumu yaweza ikawa,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Neema watakwambia, sumu unalohofia,
Na wasomi wenye gia, digrii kuning'inia,
Ukweli watakuapia, bila ya kufikiria,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Kila aliye na njaa, rahisi hununuliwa,
Usomi kweli kajaa, lakini tumbo lalia,
Huikubali nazaa, hata uhai kutoa,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Wakubwa huchaguliwa, kama ni mbovu kofia,
Matundu tele yajaa, kitu haiwezi zuia,
Wanaloliangalia, ni posho kuipokea,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Wajumbe wanunuliwa, kama gunia la mkaa,
Ni moto wa kupikia, chakula chake hadaa,
Kisha wanapo9vimbiwa, kutapika si kinyaa,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Kamba inaning'inia, hakuna wa kuifwatia,
Katikati yaishia, yawezayo sadia,
Na mkoa na wilaya, ni mizigo imekuwa,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Ni gesti za kulalia, maofisi yamekuwa,
Nani wa kufuatilia, yale yanayoamuliwa,
Kama vile wangojea, mamajusi kuingia,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Nje wanaotakiwa, ofisini wamekaa,
Ustawi wangojea, wenyewe utatokea,
Maajabu yalokuwa, 'Gordon' kutokea,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Wengi kazi ni kunawa, wangoja kupakuliwa,
Kula kwao majaliwa, na ugumba ni tabia,
Kipato chadidimia, wakwambia kinakua,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Mengi watasingizia, na yote nayakataa,
Si kweli ninatambua, mengine wasingizia,
Hakika hawajajua, nasibu wajitajia,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Mimi ninalolijua, ni njaa inayokuwa,
Pande zote kuenea, wa chini wakaumia,
Na juu washikilia, kula kama vile jaa,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Hali ikiendelea, Tsunami yakaribia,
Na wala sintoshangaa, makubwa kuyasikia,
Jumlisha na balaa, haitakuwa nazaa,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

Isiwe adui wewe, unisingiziye miye,
Mnyonge unionee, wanene wakutumie,
Kuna ngwaa kuna ngwee, majibu yake ujuwe,
Isiwe adui wewe, wadanganya  yule kule ?

No comments: