Wednesday, October 31, 2012

Ung'eng'e anayetia


TAHADHARI naitoa, kwa wasomi Tanzania,
Na wabunge nao pia, vikaoni wakikaa,
Kiingereza kutumia, lugha yenu mwabakia,
Ung'eng'e anayetia, kiswahilini abaka !

Toka sasa kutambua, kamusi twandikiwa,
Lugha yetu kuijua, kila neno kutumia,
Vipi mnayatumia, maneno yasiyokuwa ?
Ung'eng'e anayetia, kiswahilini abaka !

Kisomo shaka chatia, kila ninapowasikia,
Wasomi mngelikuwa, maneno mngeyajua,
Kila lugha kutumia, yake yanapotakiwa,
Ung'eng'e anayetia, kiswahilini abaka !

Uvivu mkijitia, hadhi mnajishushia,
Ni watu wa kuilea, lugha yenu ilokuwa,
Nyie mnaichezea, na kufifanzia mzaha ?
Ung'eng'e anayetia, kiswahilini abaka !

Kila nikiangalia, methali naikubalia,
Miti kweli pakijaa, wajenzi mtafulia,
Ndicho kinachotokea, hapa kwetu Tanzania,
Ung'eng'e anayetia, kiswahilini abaka !

Kwani twayakimbilia, kitu yasiyotufaa,
Kisha tukayaachia, thamani yaliyokuwa,
Utadhania vichaa, au ndio twalaaniwa?
Ung'eng'e anayetia, kiswahilini abaka !

Ung'eng'e sijakaaa, wenyewe kuutumia,
Nafasiye kuchukua, pale pakustahilia,
Ila sio kuchagua, lugha ya kujitegemea,
Ung'eng'e anayetia, kiswahilini abaka !

Barru kutuangazia, Mushawari wa kung'aa,
Nuru machoni kutia, la kwetu kuangalia,
Si kidogo ilokuwa, kwayo mbali twafikia,
Ung'eng'e anayetia, kiswahilini abaka !


No comments: