Tuesday, October 16, 2012

Wazee mwaaibika



WAADHIMU mnatakiwa, kwanza kuwa Watanzania,
Uchama ukafatia, na huko mnakotokea,
Vingine mkifuatia, vijana kutoelewa,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Tukilitoka mwajua, mbona dira mwakataa?
Hivi chini mmekaa, hali kuifikiria,
Au sawa mwadhania, vitu vinavyojiendea?
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Hadhi mnayotakiwa, si uchama kujaliwa,
Nyie ni Watanzania, kuongoza mwatakiwa,
Itikadi kuzipaa, juu juu kuelea,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Kila mnapofikiria, kufikiri Tanzania,
Vingine kutoamua, ila nchi kuifaa,
Vingine mkiamua, mtaiponza Tanzania,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Mafao mnayopewa, yanatoka Tanzania,
Sio chama chawafaa, hilo mngelitambua,
Wengine wakiingia, mkwara mtachukua,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Demokrasia dawa, bure mkiikataa,
Nyingine haitofaa, taifa litaumia,
Laiti mkiyajua, msimamo mtajua,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Siasa sio sanaa, kitu cha kujipitia,
Mtazamo watakiwa, na didra kuzitumia,
Vinginevyo 'kitokea, taifa wenda potea,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Budi mngepigania, bunge lenu kupatiwa,
La wazee wa kujua, nyadhifa mliopitia,
Katiba kuwatambua, maamuzi mkitoa,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Marais mmejaa, wa Bara na Zanzibar,
Mawaziri nao pia, ndani humo wangetiwa,
PIa wakuu wa mikoa, na wilaya walokuwa,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!

Na makatibu wakatua, wa wizara na mikoa,
Na mameneja wafaaa, bungeni wakaingia,
Kampuni walolea, na sifa kujipatia,
Kwa kuulea uchama, wazee mwaaibika!




No comments: