Sunday, October 7, 2012

Mwalimu anauliza



Mwalimu kaulizia, na huku akishangaa,
Cheo wanaogombea, kama vile haramia,
Wanachokikimbilia, hivi nyie mwakijua?
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Usia katuachia, b ado tunauchezea,
Na haya wasiokuwa, wajifanya kutosikia,
Mizimu yatushangaa, tuna nini Tanzania?
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Tuliokuwa wajamaa, ubepari twavamia,
Kisha sumu zake pia, nazo tunajivunia,
Muda haitochukua, tutaanza kujiua,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Wenzangu nawashangaa, kwa uziwi kujitia,
Japo macho tumepewa, upofu tunanuia,
Nchi tunaiachia, kwenda tusikokujua,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Msidhani mwajifaa, kumbe mwenda kujivaa,
Adhaniaye kavaa, kumbe uchi  atembea,
Kichekesho kukizua, kwanye mitaa na njia,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Fahari aibu kuwa, heshima kujishushia,
Mwanzo tulikoanzia, watu wema twadhaniwa,
Wakorofi kuja kuwa, twaongozwa na vichaa,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Busara tukitumia, kuna watu wanafaa,
Bila ya kuangalia, chama gani atokea,
Amani tukaioa, na umoja kuuvaa,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Vingine ninahofia, bomu tukilichagua,
Lenye uchu na tamaa, urais kuchukua,
Kumbe linajiandaa, vitani kwenda tutia,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Bomu lakununuliwa, na mabwana kuwafaa,
Vyetu wakavichukua, wengine kuwapatia,
Na utu kuukimbia, uhayawani kuwaoa,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Danguro ikulu ikawa, kwa miaka si masaa,
Waingie wasofaa, wakatoka wa kufaa,
Wakawa na changudoa, maamuzi wayatoa,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Tumuombeni Allah, nusura kutupatia,
Yakizuka ni ukiwa, nchi tutaikimbia,
Hatima ya Tanzania, Nyerere anaijua,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

Hatima ya Tanzania, Nyerere anaijua,
Viongozi wasofaa, taifa wataliua,
Na bora tukichagua, Afrika kuwa taa,
Mwalimu anauliza:
Wakimbilia Ikulu, hivi watafuta nini ?

No comments: