Sunday, October 7, 2012

Sura za televisheni




Sana ukiangalia, hili utaligundua,
Wapendao angaziwa, udhaifu wamejaa,
Nuru ikashopotea, mwanaga wanaununua,
Sura za televisheni, kuongoza hufulia!

Kila nikishuhudia, kwanguu kama ni udhia,
King'amuzi huchomoa, katuni kuangalia,
Ya uongo kushangaa, kama kweli yanakuwa,
Sura za televisheni, kuongoza hufulia!

Wabwabwaja wasojua, wala  kuyakadiria,
Mvua zikajakataa, na jua kupalilia,
Masika kushtukia, kiangazi kimekuwa,
Sura za televisheni, kuongoza hufulia!

Gele nilishaambiwa, gonjwa linanisumbua,
Nakala najisomea, lipi jipya wanazua,
Kila nikiangalia, naona wafadilia,
Sura za televisheni, kuongoza kufulia!

Nako kule nachopoa, wao wanaona poa,
Waishia kukohoa, na kuwabana vifua,
Haki isipotangulia, dhuluma hupalilia,
Sura za televisheni, kuongoza kufulia!

Watu ukipendelea, wenyewe hukuumbua,
Sifa wakajisifia, zawadi kutapikia,
Ikawa sasa kinyaa, watu kutovumilia,
Sura za televisheni, kuongoza kufulia!

Ndivyo inavyokua, swahibu nakwambia,
Ujuzi sio mazawa, kama haukujaliwa,
Na umri kweli dawa, hupona wakiugua,
Sura za televisheni, kuongoza kufulia!



No comments: