Sunday, October 7, 2012

Hali ya hewa

Kuna pepo na dhoruba, tufani nazo mvua,
Na isiyo shwari Ghuba, karibu isiyokuwa
Zikichelea msiba,  unaowanyemelea,
Hali ya hewa si njema, udikteta wachipua ?

Kuna gharika mraba, Marikani yatokea,
Obama alikoziriba, na waliomtangulia,
Hakitojaa kibaba, kwanza wao watatwaa,
Hali ya hewa si njema, udikteta wachipua ?

Urani ina janaba, tohara wapakazia,
Kwa wajinga wanaimba, nyimbo wasizozijua,
Ndotoni wakiwakaba, kizazi kukichimbua,
Hali ya hewa si njema, udikteta wachipua ?

Twashindwa vyoo kuziba, uranium kuchimbua?
Hiyo haijawa shaba, imewazidi tamaa,
Twautafuta msiba, kwa wenigne kwenda kuwa?
Hali ya hewa si njema, udikteta wachipua ?

Mabomu wakuziribwa, wengine hawatakuwa,
Kwetu wana ukuraba, ndiko watapoanzia,
Somalia wanayashiba, sisi ni kuyangojea,
Hali ya hewa si njema, udikteta wachipua ?

Kisipotosha kibaba, ukawa walia njaa,
Hautokuja ubwabwa, mauti huweza ingia,
Mikoba ameibaba, ya roho kuja  kutoa,
Hali ya hewa si njema, udikteta wachipua ?

No comments: