Wednesday, October 31, 2012

Enzi hizi za vitendo

MANENO hayamezeki,  za vitendo enzi hizi,
Mizigo haibebeki, wahitajika watenzi,
Jamii ni ushiriki, kwenye kula nazo kazi,
Enzi hizi za vitendo, hayamezeki maneno !

Imetaliki ashiki, watu wangoja mandazi,
Wamechoka unafiki, wa vitumbua vya nazi,
Waisubiri mikiki, na wao  wawe wakwezi,
Enzi hizi za vitendo, hayamezeki maneno !

Hali hawaiafiki, mkao chini ya ngazi,
Ya juu hayaharibiki, wamejaa watengezi,
Huko hawaamainiki,  walo juu yake ngazi,
Enzi hizi za vitendo, hayamezeki maneno !

Ya sasa hawabariki, yamejaa makunyanzi,
Lisemwalo si tawfiki, ni wali hauna nazi,
Si udugu si urafiki, hili haliwatandazi,
Enzi hizi za vitendo, hayamezeki maneno !

Zinadhoofu milki, na kuzizima mapenzi,
Mioyo haishtuki, chazuka kigugumizi,
Wa hariri ni kaniki, na kingine hakiwezi,
Enzi hizi za vitendo, hayamezeki maneno !

Wanazuka mamluki, kuuza kiso saizi,
Riziki kutamalaki, asiyotoa mwenyezi,
Uroho wayabariki, hata kwao viongozi,
Enzi hizi za vitendo, hayamezeki maneno !

Wake hawaaminiki, wawadaka wachuuzi,
Fedha wanaomiliki, wakifanza manunuzi,
Wanoni ni washiriki, na wanyonge wana genzi,
Enzi hizi za vitendo, hayamezeki maneno !

Hali yakwaa kisiki, manusura ni mwenyezi,
Nchi hairehemeki, yafulia matumizi,
Malengo hayabebeki, hawawezi viongozi,
Enzi hizi za vitendo, hayamezeki maneno !

No comments: