Sunday, October 7, 2012

Wakati nakuchukua



Ajabu haijakuwa,  kuifungua tabia,
Mbona hayo nikijua, subira nikaamua,
Vazi nilishakuvua, ngozi ya mbuzi ukiwa,
Wakati nakuchukuwa, nilikuwa nakujuwa !

Dawa ulizotumia, mbona nilishaanguliwa,
Ushirikina nazaa, kwangu ni usioingia,
Ila ninachoamua, mwenyewe ninakijua,
Wakati nakuchukuwa, nilikuwa nakujuwa !

Kuteka ulidhania, mateka umepatia,
Mfukoni kunitia, na amri ukazitoa,
Nami nikikuitikia, ukadhani wayajua,
Wakati nakuchukuwa, nilikuwa nakujuwa !

Muda nilikuachia, upepo wanipepea,
Subra sikuachia, mvumilivu nikawa,
Wala sikukuchimbua, kukutafuta ubaya,
Wakati nakuchukuwa, nilikuwa nakujuwa !

Siku ninaingojea, kamba kujaachia,
Salama itapokuwa, kwa wana wanaokuwa,
Pembeni kujiangalia, na Molal nikamrejea,
Wakati nakuchukuwa, nilikuwa nakujuwa !

Pembeni kujiangalia, na Mola kumrudia,
Ndiye amenifungua, haya ninayoyajua,
Shukrani kuzitoa, uchamungu naamua,
Wakati nakuchukuwa, nilikuwa nakujuwa !


No comments: