Sunday, October 7, 2012
Sio vyote huchanua
Nchi inaelekea, kwenye uongo kuvua,
Na majoho ya hadaa, kichakani kwenda tupwa,
Uzaini kuutoa, na ukweli kupumua,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Ni vingi waviandaa, ili watu kuhadaa,
Wakiona vinang'aa, uzuri kuudhania,
Kwao wakavifatia, shimoni kutumbukia,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Mbegu wanaziandaa, wapate kujipandia,
Chini zitaozea, na baadhi kuchipua,
Kwalo wakajisifia, watu wawasaidia,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Tutaona zachipua, kila kona Tanzania,
Hasa wasikotakiwa, na ahadi wametoa,
Na wajumbe wamevia, wengine kununuliwa,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Maji yatawaishia, washidwe kunyweshea,
Na miche ikajifia, udogoni ilokuwa,
Vigumu kuendelea, ukame ukizidia,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Sasa wanajititimua, utadhani wamejaa,
Kumbe wamepuliziwa, ni pulizo lililojaa,
Sindano yakimbilia, si muda kuwatoboa,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Mpasuko kitokea, wote tutalisikia,
Wako watakaokimbia, na wengine kujifia,
Bomu wakalishangaa, kutoka wasikojua,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Hofu ninawahofia, wote wasiojjua,
Kushika kisichokuwa, mikongo wakang'olewa,
Na haramu kuchagua, dhambi wakajibebea,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Halali watakimbia, haramu wakachukua,
Na wakija kugundua, muda umeshapotea,
Laiti sasa ikawa, kitu kisichotokea,
Ukiona vyachipua, sio vyote huchanua!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment