Sunday, October 7, 2012

Sio mbio za vijiti



Nani amewaambia, eti mbio twakimbia,
Za vijiti kuchukua, wa mbele kumpatia,
Mikia kung'ang'ania, nafasi kwenda zizoa,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Na sasa wazitimua, wengi wakisiginia,
Na njumu walizovaa, vidole zatutoboa,
Imekuwa ni balaa, wenzao washangilia?
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Pumzi wanakwapua, na vidonge kutumia,
Mapafu yamewajaa, ya kishetani furaha,
Vumbi dhambi limejaa, poda wanatuambia,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Hata nami nashangaa, riadha inayokua,
Za kweli wanafulia, za uongo wanazua,
Bayi keshawaambia, uongo wasingizia,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Hii nchi ya mafua, hakuishi kukohoa,
Dawa sasa za bandia, umauti watu'zia,
Ukatanda na ukimya, chanzo chake kukijua,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Wenyewe wajichagua, nasaba kuendelea,
Fukara kasahauliwa, na chama kilichomzaa,
Mitaa yamngojea, umatonya kwenda kuwa,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Katika kuendelea, mbio zinapokelewa,
Na chaji waliotiwa, umma kutumikia,
Mbio wanapotimua, ubinfsi hujikwaa,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Watu ukitegemea, mbali wakumalizia,
Shaka ukishatambua, salama utaijua,
Wa Ulaya wanajua, milango nanga watia,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Wa Ulaya wanajua, milango nanga watia,
Ili unapogongewa, nusunusu kufungua,
Mtu ukishtambua, ndio kumkubalia,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Majoho yatawajia, na hata suti mpya,
Thamani kuigundua, huwa ni kubwa nazaa,
Mtu huwezi mjua, ila akikutumikia,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Undani ukimjua, nusura huiambua,
Kamili hatokuwa, lakini hatopwelea,
Kadiri ataachia, mbele ukajisongea,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

Sasa kujifaragua, ukweli mkaujua,
Ukubwa wanaolilia, nyayoni wanaishia,
Machimboni mwatakiwa, kwenda bora kufukua,
Sio mbio za vijiti, fani mbio kupeana!

No comments: