Wednesday, October 31, 2012

Silaha za sikuhizi



Zamia ukaijua, juu huachi kupaa,
Inakokwenda dunia, tekhohama silaha,
Mwana unapomlea, mpe nakupa nasaha,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!

Mengineyo ni udhia, maoboti watakiwa,
Njiani wakaingia, machozi wasiolia,
Pilipili wasojua, na kudhuru haijawa,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!

Sasa watu wanakaa, majumbani kutulia,
Vitufe wakatumia, ndege juu zikapaa,
Na kama walivyo njiwa, ujumbe wakachukua,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!

Wenda mbali kwa kupaa, silaha ndani zajaa,
Na huko ulikokaa, unaweza kufyatua,
Shabaha ukitumia, hakuna wa kubakia,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!

Mamake teknolojia, silaha zinazofaa,
Akili zinatumia, sio nguvu kutumia,
Na kila anayejua, hatua anachukua,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!

Elimu inatakiwa, si ujinga kuulea,
Nyuma anayebakia, atakuja kufulia,
Angani zinaingia, akili zajibangua,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!

Humhehimu dunia, mbinu anayezijua,
Ujinga anayelea, utumwa huendelea,
Kuamka yatakiwa, muda  kuusakazia,

Juhudi inatakiwa, wenetu kukumbatia,
Wapate teknolojia, na vyema kuitumia,
Pamwe na kuwa silaha, lugha itatujengea,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!

Tumuombeni Jalia, macho yetu kufungua,
Hili juu walijua, sikunyingi watumia,
Nanyi mliochaguliwa, mwatakiwa kuelewa,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!

Kitabu mkiingia, miraji mtaijua,
Ahlil kitabi radhia, nani asiyelijua,
Ila wanaojizuzua, na kujifanza wajua,
Silaha za sikuhizi, mamake teknolojia!



No comments: