Sunday, October 7, 2012

Ya halali hawawezi


Katika dunia hii, isyo na mang'amuzi,
Iliyojaa jinai, tunguri na mahirizi,
Tabia stihizai, wabeba hawajiwezi,
Ya halali hawawezi, wakimbiliao siyasa!

Katika dunia hii, yenye rushwa na uwizi,
Si ridhaa kukinai, uachie king'anuzi,
Wenzako watakurai, hata kama hauwezi,
Ya halali hawawezi, wakimbiliao siyasa!

Katika dunia hii, ya unafiki si mapenzi,
Shaytwani anafurahi, kujifunza kwa wazuzi,
Haombi tena utii, kwenda kwake ndio ngazi,
Ya halali hawawezi, wakimbiliao siyasa!

Katika dunia hii, ya ushuzi na upuzi,
Vyeo sasa kwa karai, wapewa waso makuzi,
Ni mradi wa uhai, riziki za kubarizi,
Ya halali hawawezi, wakimbiliao siyasa!

Katika dunia hii, vitumbua si mandazi,
Mchele watanabahi, kuwa uji si ujuuzi,
Kila mwenye kujistahi, budi kuwa mdokozi,
Ya halali hawawezi, wakimbiliao siyasa!

Katika dunia hii, yenye giza na ushenzi,
Na uuongo wa madai, kulipwa bila ujenzi,
Nchi ina jitimai, bila kutoa machozi,
Ya halali hawawezi, wakimbiliao siyasa!

Katika dunia hii, ya kula na matanuzi,
Roho njema huzijui, hadi uwe mwangalizi,
Jambo jema situmai, hata kwa walio wapenzi,
Ya halali hawawezi, wakimbiliao siyasa!

Vipaji tumekinai, kwa hila na ubaguzi,
Dhuluma tunaitii, na shari kwetu ni radhi,
Inafika asubuhi, itaponguruma ardhi,
Ya halali hawawezi, wakimbiliao siyasa!

No comments: