Sunday, October 7, 2012

Usalama wa kichama


Si salama ni balaa, usalama wa kichama,
Cheche wakishuhudia, hilo bomu watasema,
Hofu imewaingia, wakihofia kiyama,
Usalama wa kichama, si salama ni nazaa!

Viumbe huvitumia, visivyo nayo huruma,
Hata watu wakaua, na uoongo kuusema,
Ni nani asiyejua, wakosao taadhima,
Usalama wa kichama, si salama ni nazaa!

Uhuru pasipokuwa, huwa hakuna salama,
Wenye shibe hutumia, wenye njaa kuwatuma,
Nchi kuchokonoa, hadi isiwe salama,
Usalama wa kichama, si salama ni nazaa!

Yameanza kutokea, na sasa tunayasoma,
Walianza kuzomea, na vigelegele kukama,
Na kwa leo twajifia, kwa hiyo yao adhama,
Usalama wa kichama, si salama ni nazaa!

Nchi juu yatakiwa, ndio tukawa salama,
Vingine tutafulia, kuuana ni lazima,
Macho msipofungua, tutaipata nakama,
Usalama wa kichama, si salama ni nazaa!

Watu tukiwaachia, wakaifanza dhuluma,
Hali tunaangalia, pasipo ya kulalama,
Wakati hufikia, tukazua uhasama,
Usalama wa kichama, si salama ni nazaa!

Maovu yatachipua, pasibakie salama,
Kwa kushoto na kulia, mambo yakenda mrama,
Walaji kufurahia, na fedha nje kutuma,
Usalama wa kichama, si salama ni nazaa!

Hadhi ikatukimbia, kisiwa kiso salama,
Maovu yazidi kujaa, kwenye nchi navyo  vyama,
Na mengine kuyazua, ikafuatia nakama,
Usalama wa kichama, si salama ni nazaa!


No comments: