Sunday, October 7, 2012

Demokrasia si nusu



Nusu mkiichukua, basi nusu hubakia,
Watu wakaitezea, huku mambo wafulia,
Ngome wakazitumia, na nyufa zilizozidiwa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Pakiwa kuabudiwa, huvia demokrasia,
Katu haitochanua, kitanzini mwajitia,
Siku huja kufikia, hasama mkazizua,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Juu anayetakiwa, si rais ni raia,
Kisha wote kuwa sawa, chini ya zao sheria,
Mmoja juu akiwa, katiba yenu ni mbaya,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Iwe rahisi kumtoa, unapozidi udhia,
Umma unapoamua, kwa vyombo kuvitumia,
Kanuni zikatungiwa, hadaa kuziondoa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Tume inayotakiwa, ni huru iliyokuwa,
Sio kesho kuanzia, hivi sasa yatakiwa,
Vinginevo inakuwa, watu wanahujumiwa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Ni uwizi unakuwa, wa mchana ulokuwa,
Huku wanaangalia, hao wlaiodhaminiwa,
Kuihoji yao nia, mtu hvi atakosea?
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Polisi wanatakiwa, kusoma demokrasia,
Fursa kuitambua, huru yao tasnia,
Na mwiko kupendelea, au kwenda nunuliwa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Kama kwenye mizania, usawa kuutumia,
Pamwe kutowaonea, na nguvu wasiokuwa,
Huku wakitegemea, kwalo kwenda zawadiwa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Dunia  mkiangalia, kasoro mtazijua,
Nusu iliyofifia, leoo wanajiumbua,
Kwa mfano Syria, na Kenya tunayajua,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Zimbabwe yanatokea, na  kusini nako pia,
Yawashinda Nigeria, yalivyowageukia,
Mwanya walipoachia, mpasuko watokea,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Kongo yazidi fulia, kwa unafiki kujaa,
Burundi na huko pia, salama haijakua,
Uganda yajiumbua, nafaisi kuichezea,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Afrika nawaambia, nusunusu huumbua,
Mabaya nawaotea, asubuhi kuingia,
Mbali hamjafikia, mkalaumu kifaa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Kifaa demokrasia, vizuri kikitumiwa,
Hupanga na kupangua, haki ikazitambua,
Mizani kutosinzia, upande kuhujumiwa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Kifaa demokrasia, kikienda kwa usawa,
Hakuna wa kuumia, watu watafurahia,
Leo kinachopotea, kwa uzuri kutumiwa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

Kifaa demokrasia, utata kisipokuwa,
Serikali itakaa, yake kutopanguliwa,
Vyama viwe vaingia, na salama kuvitoa,
Demokrasia si nusu, kamili yahitajika!

No comments: