Wednesday, October 31, 2012

Tatizo si uongozi



Utakwepo uongozi, huu ukiisha kazi,
Kwa hiyo ya uongozi, Katu hayatutatizi,
Ila ni ya viongozi, wanaofanza ajizi,
Tatizo si uongozi, tatizo ni viongozi !

Uongozi kama ngazi, ni kitu cha matumizi,
Asiyekuwa mjuzi, kuipanda kuna kazi,
Kuanguka kuko wazi, akashikwa kigugumizi,
Tatizo si uongozi, tatizo ni viongozi !

Watu wana zao hadhi, kwenye safu uongozi,
Kuna bora kiongozi, mradi kiti kaenzi,
Na uongozi azizi, unaisadifu ngazi,
Tatizo si uongozi, tatizo ni viongozi !

Muihesabu miezi, ya kutafuta walezi,
Fedha wasiokabidhi, ili waipate kazi,
Ila wanaomaizi, kufaa watu ndo kazi,
Tatizo si uongozi, tatizo ni viongozi !

Huwa hawajitangulizi, nyie huwa watangulizi,
Yao kwao sio wajenzi, hadi kwanza muwe wajenzi,
Chenu hawakinguzi, kuongeza ndio radhi,
Tatizo si uongozi, tatizo ni viongozi !

Yao hawayasogezi, hadi mnao ujenzi,
Kisha yakawa makazi, na riziki yawaezi,
Ndio hufata mapenzi, kutafuta utowezi,
Tatizo si uongozi, tatizo ni viongozi !

Hawakimbilii enzi, wanatafuta ujenzi,
Wawajenge kwa makazi, na utu ni yenu hadhi,
Kisha ndio wadarizi, mengine kujabarizi,
Tatizo si uongozi, tatizo ni viongozi !

No comments: