Sunday, October 7, 2012

Maneno umetamka



Neno huwa laumbika, japo wafanza dhihaka,
Siku yake ikifika, utaiona hakika,
Kulia au kucheka,bado ya kueleweka,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!

Ulimi umetamka, mbinguni yamesikika,
Huwahi linalofika, na pale likapangika,
Kama ndilo walitaka, mara lako hugeuka,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!

Firauni katamka, nalo likasadikika,
Na katika hii miaka, ibra yaja kuzuka,
Na mwendo tunaoutaka, huenda kubadilika,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!

Asiye na mshirika, utani huuzunguka,
Kiuno ukageuka, nyuma kwenda kutundika,
Ndivyo watu hujizika, hali hai wabebeka,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!

Imani moyo yataka, na matendo kujengeka,
Na kila anayeubaka, hujing'ata kwa mashaka,
Siku zinapofutika, kweli ikadhihirika,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!

Udhalili naushika, ujibari sijataka,
Sijui ninakofika, nan mwendo si wa hakika,
Wala sintokereheka, subira nimejivika,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!

Sijigeuzi ni duka, bidhaa nikafurika,
Nachagua la kukoka, mengine ninayaweka,
Na saa inapofika, kamandua huombeka,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!

Unyonge naufutika, kwenye ala ya uoka,
Hapa uliponishika, kwa mkate natosheka,
Na kibanda naridhika,
hekalun sijalitaka,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!

Dunia kwangu wahaka, walan sio wakawaka,
Hapo nilipopafika, sikuwa nayo hakika,
Namtukuza Rabuka, mtoa asiyelipika,
Maneno umetamka, kayasikia Rabuka!



hatma collection leaflet

No comments: