Sunday, October 7, 2012

Nilikuwa na hofu ...


Saiti toka nyikani, yangu kubwa haikuwa,
Na walio na imani, nao kimya walikaa,
Ikajiri nuksani, hata watu kuuawa,
Wachamungu nilihofu, nchini wamepotea!

Fisadi waliwalaani, hata nje kusikia,
Kuzuka kwa muumiani, wao kimya wakakaa,
Na leo tu taabani, twatakiwa kujijua,
Wachamungu nilihofu, nchini wamepotea!

Namshukuru Manani, kilio kimesikiwa,
Wenye imani ya kweli, shari wameshagundua,
Si mitume wasanii, kiyama wafurahia,
Wachamungu nilihofu, nchini wamepotea!

Ilinishinda imani, moyo vigumu kutua,
Mengi kichwani kudhani, wote tumenunuliwa,
Na mboga ya mgagani, sote tunyotumia,
Wachamungu nilihofu, nchini wamepotea!

Niliikosa yakini, na hekima kutojua,
Nikajihisi amini, nami nimeishapotea,
Nimetolewa kundini, kwa hisabu kutotiwa,
Wachamungu nilihofu, nchini wamepotea!

Niliona niko chini, hakuna wa kuninyanyua,
Na mzigo u kichwani, hakuna wa kunitua,
Na kesho sikuamini, kuwa nitaifikia,
Wachamungu nilihofu, nchini wamepotea!

Nilistawi akilini, na pumzi kuzitwaa,
Kauli sikuamini, mara nilipoisikia,
Nikajiona mtani, mzaha nimeshafanziwa,
Wachamungu nilihofu, nchini wamepotea!

Taarifa sikioni, neno moja kusikia,
Nikafufuka imani, na kazi kushangilia,
Hivi niko duniani, na wema  wangali pia?
Wachamungu nilihofu, nchini wamepotea!



No comments: