Wednesday, October 31, 2012

Katikati usikae



 Yaamka Tanzania, bora yataka chagua,
Na mapema kuamua, na wewe utajaliwa,
Mwanga ukautambua, na giza kuligundua,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, wewe mtu wa rushwa, au rushwa wakataa ?

Kuna wanaokubalia, rushwa sasa wanalea,
Ukitaka kumbatia, hilo umeruhusiwa,
Ila baya linaua, na ni gumu kulilea,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, wewe mtu wa rushwa, au rushwa wakataa ?

Tume huru yatakiwa, kabla chaguzi kwingia,
Hakuna la kungojea, ila kufanza hadaa,
Ni rahisi kuamua, rais akiamua,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, tuanze badilika, au tungoje katiba ?

Kuna vyombo vya sheria, batili waichagua,
Liso haki laridhiwa, la haki kukataliwa,
Mwananchi ni kuamua, ni lipi unaridhia,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, waitaka batili, au wataka halali ?

Watu wanawanunua, kwa kushoto na kulia,
Watakiwa kuamua, kama hili waridhia,
Na kama walikataa, sauti yako kutoa,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, waitaka batili, au wataka halali ?

Wazuka Watanzania, wenye uchu tamaa,
Uroho pia na njaa, kesho kwenda chaguliwa,
Na wanaloligembea, hakuna anayelijua,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Watu sawa kununua, au dhambi kununua ?

Kuna wanaotuambia, magari ni kuendelea,
Nyumbani twafa kwa njaa, kitu gani kutufaa,
Kama washangilia, kibwebwe kujifungia,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, magari ustawi, au manufaa nyumba ?

Eti wanatuambia, vitu ni kuendelea,
Ulaji wauchochea, hata hela 'sipokuwa,
Madeni kuja tutia, kama Giriki tukawa,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, magari ustawi, au manufaa nyumba ?

Mafuta tukipatiwa, na madini yalokuwa,
Sera inayotufaa, ni elimu kugharamia,
Tutaujenga usawa, mbio pakuzianzia,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, elimu yetu bure, au lazima kulipa?

Tiba inatuchengua, bure bora kuitoa,
Inaongeza usawa,  unyonyaji kupungua,
Debe ninaipigia, jamii kusaidia,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, tiba yetu bure, au shuruti kulipa?

Michezo tunafulia, wote tunajionea,
Nani wa kugharamia, vijana wapate kua,
Ovyo tukiliacia, arijojo litapaa,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, tufadhili michezo, au tufadhili fisadi ?

Fedha shetani balaa, huru ukimuachia,
Minyororo kututia, tusokuwa na tulokuwa,
Yatakiwa kuamua, vipi tunachukulia,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, fedha itutawale, au tutawale fedha?

Ubeluskoni nazaa, vituko tutashangaa,
Langu ninaloamua, watu pesa kukataa,
Hao ni maharamia, wanasiasa hawajawa,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, fedha itutawale, au tutawale fedha?

Wapo waliotulia, katikati wamekaa,
Tunawajua tabia, sio watu wa kutanua,
Na cheo wakipewa, kichwani hakitaingia,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, fedha itutawale, au tutawale fedha?

Uongo tumechagua, mengine kujifanzia,
Imetuzidi hadaa, sasa inatuumbua,
Lazima kufikiria, bora tukaliamua,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, uongo wakubali, au wataka ukweli ?

Na bora kuliamua, ni uongo kukataa,
Mola hatoliridhia, ukweli tukiachia,
Taifa litadumaa, nidhamu tusipotia,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, uongo wakubali, au wataka ukweli ?

Maisha tukiamua, busara inatakiwa,
Upande kuegemea, usiokuwa na mbawa,
Sera hizi nazijua, babu alikizitumia,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, wala na matajiri, au wala na fukara ?

Vijiji vinatakiwa, nchi yetu kukomboa,
Nyumba tukiwajengea, utalii utakuwa,
Akili tukitumia, mengi twaweza kuzua,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, waozssha vijiji, au walea vijiji ?

Ubia unatakiwa, kilimo kuendelea,
Vijji vikaingia, na tajiri walokuwa,
Wao jasho wakatoa, na mgeni ni vifaa,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, waozssha vijiji, au walea vijiji ?

Uvuvi hivyo ukawa, wanavijiji kupaa,
Pwani wanaokaa, kunakotisha kwa njaa,
Haya tukiyaamua, nchi itaendelea,
Upande upi chagua, wewe mkono waunga;
Katikati ukikaa, historia ya kuzika:
Je, waozssha vijiji, au walea vijiji ?

No comments: