Wednesday, October 31, 2012
Yao wanapoyapanga
NAWAONEA huruma, akili wanaojitia,
Wakaifanza dhuluma, mbele kutofikiria,
Kielimu wanakwama, njia hawajaijua,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Hii ni kubwa kalima, milango inayofungua,
Mambo mengine adhama, stahi yahitajiwa,
Yasijeenda mrama, ikawa ni kulaumiwa,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Mambo yataka rindima, na mtoa wamjua,
Mpangaji mwenye hima, hakuna asichojua,
Huna siri kumnyima, aache kuitambua,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Majinaye ni Alima, ilmu aiandaa,
Nasi wote maamuma, lake tunalingojea,
Hata ukiona ngama, angani wanaoingia,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Akili kawaazima, za kwao wakajitia,
Hiyo ni yake rehema, vya kwake kuvitumia,
Hana anayemnyima, kutafuta akiamua,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Walio kwetu zahama, wasotaka tangulia,
Waturudishao nyuma, wengine kutegemea,
Hadimu hawajahama, wazaliwa Tanzania,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
NI watu wa kukoroma, na uongo kutetea,
Ila lililo na uzima, huwa wanalibagua,
Uungu wesha uazima, kitu gani kuwambia ?
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Huwa wazaa tuhuma, kuishi kama vichaa,
Vizuri ukiyasema, ubaya watautia,
Ukiwafunza kuchuma, wao watajiibia,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Watu wa kurudi nyuma, wengine huwasifia,
Ajabu yao tazama, yao watapuuzia,
Mchezo wao zahama, na adui kuhofia,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Watu wa kurudi nyuma, hawawezi tangulia,
Enzi zao za lawama, na mchawi kumgundua,
Kwao hufua hekima, wakaanika udhia,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Watu wa kurudi nyuma, lugha yao hufulia,
King'eng'e wakakisema, hata kisipotakiwa,
Maovu yanayofumwa, ulemavu huwatia,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Hukimbilia kukama, nyonyo hawajui njia,
Na teke likituama, samadi huangukia,
Akili ni kuazima, kama usipojaliwa,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Kama simba 'ngenguruma, vigumu kunisikia,
Watu wa kurudi nyuma, kushindwa wanakataa,
Wahakam wao mgema, nazi asiyeangua,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Hawaamini kiyama, hadi kinapotokea,
Watu wa kurudi nyuma, siku yao husinzia,
Jibrili hatokwama, nyepesi zake hatua,
Yao wanapoyapanga, Mola naye anapanga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment