Tuesday, October 16, 2012

Laiti wangelijua

Laiti wangetambua, hili wangeazimia,
Watu wakawajengea, maadui kuwaua,
Watatu waliokuwa, ndiye wa kutegemewa,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Mengine kuwaachia, wenyewe watajifanzia,
Nyumba wakishajengewa, akili zitaingia,
Maajabu watazua, kwani wanafikiria,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Nchi kiwanja ikiwa, wote ni kujijengea,
Moja tu twaliwazia, na mengine kufifia,
Muda itatuchukua, maadui kuwaua,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Wa kwanza kumuondoa, ufukara atakuwa,
Kusepa ataridhia, afadhali  kumwachia,
Kisha akafuatia, maradhi mlaumiwa,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Kisha akafuatia, maradhi mlaumiwa,
Miundo mbinu ikiwa, uchafu inaondoa,
Usafi ukasambaa, ikawa ndiyo tabia,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Na muda utabakia, kinamama kujisomea,
Ujinga ukakimbia, huko unakokujua,
Na mama akishatambua, taifa zima hujua,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Halafu atafatia, maradhi mlaumiwa,
Nchi anayezingua, watu wetu wakavia,
Wengi wanaogua, washindwa kutuchangia,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Wao wasichoelewa, ni ajira mardhia,
Vijana kuajiriwa, kutengeneza vifaa,
Kila kimoja kikawa, mradi wa kujitegemea,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Udongo watachimbua, ajira kujipatia,
Ufinyanzi kuridhia, matofali kufyatua,
Na vigae navyo pia, wakawa wavitanzua,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Miti watainunua, Iringa kukachanua,
Milango wakaandaa, kwenye nyumba kuwekea,
Na madirisha kutoa, nakshi yaliyotiwa,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Taizi watachimbua, za vito zilizokuwa,
Sakafuni wakatia, nyumba zikapendezea,
Ni rahisi itakuwa, nchi hii kunyanyua,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Vijiji tutashitua, mara moja vikakua,
Usingizi kuondoa, wakazi kujiamkia,
Hili wakishangialia, kasi yao itakuwa,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Kasi yao itakuwa, ya kutaka endela,
Hakuna la kuzuia, umeme kudadavua,
Na maji wakachimbua, na bomba kwenda zitia,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Wapo wataopimia, maeneo kuhamia,
Eka wakaziandaa, si vidunchu kuachia,
Ili mtu kujilimia, vimbogamboga ikawa,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Viwili vitaanzia, au vitatu vikawa,
Vyumba vya kuingia, ibakie kutanua,
Mtu anavyoamua, ya kwake kuendelezea,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Ujasiriamali njia, watu wakaifuatia,
Hadi juu kufikia, na kheri kulikokuwa,
Wakawaka Tanzania, hadithi ikatimia,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

Sasa kinachotakiwa, ni uchama kuua,
Sera wanaozikataa, ambazo zinatufaa,
Waache kujishaua, ugumba wakakataa,
Nyumba dawa mujarabu, laiti wangelijua ?

No comments: