Sunday, October 7, 2012

Wazee wala maisha


Ukiangalia historia, vitani wanaoingia,
Vijana huwatumia, kama vile marisawa,
Adui akatupiwa, kuwala na kuchachafya,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Vijana nyasi wakawa, wanyama wakapatiwa,
Ni chakula cha kuliwa, ndani na nje wakawa,
Ili kuwapigania, na haki wasiokuwa,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Wazee wakichangia, wao hawatatoa,
Wa wengine huchukua, vitani kwenda uawa,
Uzalendo wakatia, neno la kutamaniwa,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Wafaao kuuawa, kwa mujibu huamua,
Masikini wenye njaa, na kazi wasiokuwa,
Wao waliojishibia, kuishi wanatakiwa,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Libya yametokea, nasi tunajionea,
Na malipo wachukua, wazee waliokuwa,
Vijanawahadaiwa, na kugeuzwa wabaya,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Syria yanaendelea, Assad ametulia,
Yeye na wake jamaa, wangali wanatumbua,
Masikini wneye njaa, ndio vita vyawatwaa,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Kaburi mtajichimbia, hivyo nanyi kuamua,
Vijana wa Tanzania, mnapaswa kujijua,
Chama kutowatumia, sumu mkainunua,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Rudieni historia, Mwalimu katuambia,
Njia akatupatia, ifaayo kutumia,
Sana walojaa njaa, uchu na kubwa tamaa,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Sana walojaa njaa, uchu na kubwa tamaa,
Ikulu kukibilia, na watu kuwanunua,
Hao ni wa  kuwahofia, taifa wataliua,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!

Haki msipojitendea, wenyewe mtaumia,
Mkabakia ukiwa, muongo hauujaishia,
Tanzania iwe kulia, 'chozi ya damu yakawa,
Vijana wanauana, wazee wala  maisha:
Ndio mchezo wa vita!


No comments: