Monday, October 15, 2012

WALIOPO WAMECHOKA



Wahitaji pumzika, akili kuzichochea,

Wameishachakarika, na wapambe wao pia,

Mengi yashindwa fanyika, watu wamejichokYea,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Wanafulia hakika, kifikra wanapotea,

Njia wanayoishika, ubayani yaelekea,

Nao hawana hakika, pazuri wanadhania,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Yanawapanda mahoka, maadui kuotea,

Na mabomu kutumika, watu wakawapofua,

Subira wanaizika, kwa maovu kuchimbua,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Kazi kulalamika, na uongo kuandaa,

Vijana mwahadaika, hawa wakiwanunua,

Azimio kutamka, uongozi kuchukua,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Wakati umeshafika, kilingeni kuingia,

Muongoze Afrika, kama Kabila kwanzia,

Nchi nzima ameshika, mtaishindwa mikoa?

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Ujana ni bora dawa, wazee mkitumia,

Wala sio kutumiwa, wakaganga yao njaa,

Kinyume mkiachia, mtakuja kujiua,

Wazee wameshachoka, sasa wanaganga njaa,



Wazee kazi yafaa, wajukuu kuwalea,

Ushauri wakatoa, na ya mbali kuwazia,

Ukuu ukiwaachia, hukataa kujifia,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Angola ukiangalia, haya utajionea,

Zimbwabwe nako pia, kizee ang'ang'ania,

Kwa haya kujikwepea, baibai kuwaambia,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Mikutanoni waingia, kuiganga yao njaa,

Akili zimepotea, vya uongo vinatiwa,

Na wakawakubalia, hasidi waliojaa,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Halmashauri waingia, ili ada kwenda pewa,

Watoto wakalipiwa, masomo kuendelea,

Waliwatuma Ulaya, hela zimeshawaishia,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Hapataisha udhia, hawa wakiendelea,

Ni watu wa kutumiwa, wengine wakadokoa,

Na macho tunajifia, vipi tutajionea,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Vijana wa Tanzania, umoja unatakiwa,

Uchama kuukimbia, udugu mkauzua,

Umoja wa Tanzania, vijana kujiundia,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Baba wanaofatia, na mama kuwalilia,

Kunyonya wasioachia, na jipya waiokuwa,

Hawa ni kuwaachia, iwafundishe dunia,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!



Kwa Mola nawaombea, muweze kufanikiwa,

Wazee kuwaondoa, ustawi mkauzua,

Na uvumbuzi nao pia, vifaavyo kugundua,

Waliopo wamechoka, waacheni wapumzike!

No comments: