Wednesday, October 31, 2012

Hii ni hotuba nzuri

NaONA wamehariri, kama wimbo imekuwa,
Mashallah tahariri, kila kitu inajua,
Ningelisema kafiri, ila neno nahofia,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Msomaji kakariri, hata walipokosea,
Inang'ara kwa dhahiri, ila feli haijatwaa,
Na nimeipata habari, watu walikisnzia,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Hotuba kama hariri, laini ilivyokuwa,
Ingelikuwa kadari, lake lingeshatimia,
Kuna vichaka na pori, msituni huishia,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Hii hotuba mahiri, ugonjwa unaujua,
Bali wesha daktari, ugenini wahamia,
Na walimu wadhukuri, kimbioni kukimbia,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Hotuba hii hodari, ila kilio yalia,
Wamezidisha hasiri, mkombozi kajikwaa,
Aogopa istifari, kwa israfu kutia,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Hotuba hii kadiri, njia inaitambua,
Isipokuwa yakiri, watuwe hawana nia,
Kuna  kitu wasubiri, na mimi sijakijua,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Hotuba hii shairi, siachi kujisomea,
Mteperevu fakiri, hekima najionea,
Na shair yazidi heri, ndilo nililiogundua,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Dariziye za fahari, na pindo zanakshiwa,
Ila kilicho sifuri, akili zinatibua,
Haujawa umahiri, ila riziki hutoa,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Tamathali zadhihiri, usawa zisizokuwa,
Dunia sasa hiari, mtu kitaka kujua,
Wapo walio fakiri, leo tajiri twajua,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Siasa si mahubiri, hotuba sasa za njaa,
Watu wanazighairi, shibe wataka sikia,
Pasipnayo ghururi, mishono watafumua,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Pepo zataka mahiri, pepezi zikifuatia,
Wakaijua hadhari, kule zinakoendea,
Na  maji haya ni zari, mtu huzama kakaa,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Hii ni mpya bahari, na weledi waijua,
Kuogelea hatari, akili usipotumia,
Mabavu ukivinjari, mwenyewe huja kulia,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

Mivumo inabashiri, pepo wasiotulia,
Kuntu wameshadhihiri, si watu wa kung'olewa,
Hawahofu majibari, wanavifua vifua,
Hii ni hotuba nzuri, kama nyimbo yaimbika !

No comments: