Sunday, October 7, 2012

Vijana mkijiuza



Wachuuzi wanatangaza, kama mwataka jiuza,
Miaka yafululiza, tanga waanza kutweza,
Njis wanayopitiza, bahari imeshaoza,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kushindwa wajikataza, ngoma hiyo kuicheza,
Wanapenda kupendeza, na ushindi wa kuzoza,
Demokrasi waiza, wataka kuipoteza,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi ni muweza, ukweli anayefanza,
Si wa ndoto kutujuza, na wengine kuchafuza,
Hirizi anayetunza, na ulafi kuukuza,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Ahadi wanaokoza, wakashindwa kutimiza,
Ukiona wawatunza, kunazo nguvu za giza,
Msidhani miujiza, mkiiza mtalizwa,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Fisadi ni wanagenza, pamoja wanafanyiza,
Nchi wameshachuuza, wanangoja kuiiuza,
Na tunzo mkiwatunza, ukweli watafanyiza,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Gharama hamtaiweza, mambo yatawatatiza,
Kazi yao ni uviza, kuzaa hawatoweza,
Nchi wataibamiza, damu wakatiririza,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, alokuwa damu mpya,
Ukale kuuachia, tupate kizazi kipya,
Hatamu kitakachokataa, na halali kuchagua,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, mchumi wa kuchimbua,
Hivyo vinavyopotea, hazina akavitia,
Wala si wa kutumiwa, dhahabu atuibia,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, umeneja wa kujua,
Mambo akatupangia, chanya yanayotakiwa,
Na sio nyingi ruia, dunia zisizofaa,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, nje wasiyemnunua,
Sumu akaja chimbua, watu wetu kuwaua,
Na miradi kufungua, mazingira isofaa,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, ukabila asokuwa,
Wao akisadia, wengine kutokuwafaa,
Kujuana na kujua, ni cheo chenye kinaya,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, udini asiyejaa,
Dini yake kuifaa, na wengine kusinyaa,
Nchi huja kuigawa, vitani mkaingia,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, waandishi asonunua,
Na redio kuitumia, yake kutangazia,
Na tivii kumtoa, hata kwa lisilotufaa,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, kisasi asiyetia,
Watu akawakomoa, na ulemavu kutia,
Nusura si wa kujua, lao wanakimbilia,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, asiyejilimbikia,
Mali akafikiria, badala ya kujitolea,
Tumbo litatangua, akili zikafatia,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!

Kiongozi atakiwa, ubia anayehofia,
Wa nje kumtumia, nchi wakainunua,
Watumwa tukajakuwa, hapa kwetu Tanzania,
Vijana mkijiuza, mtaliua taifa!




No comments: