Wednesday, October 31, 2012

Chagueni cha sitini


HAMSINI na sitini, hasra kitawatia,
Wana mengi mahumuni, haramu yaliyouwa,
Ya kwao msiamini, siku moja mtalia,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Mimi ninakikataa, kundini ijapokuwa,
Najua nimeshafulia, siwezi watumikia,
Neema sintawaletea, ni ajizi na udhia,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Wa sitini wanafaa, hamsini  wafikia,
Na akili zatulia, uzee haujakaa,
Akili watatumia, wakiridhi teknolojia,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Hamsini chafikia, ngazi bora kitakuwa,
Hakina kusingizia, uhuru kutuletea,
Au waliochipua, ukada kutumikia,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Hhamsini wanafaa, hamsini twafikia,
Mstari kuutia, kizazi  kipya kikawa,
Ya nchi kuwaachia, sio kuyang'ang'ania,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Rais mtarajiwa, teknohama atajua,
Pepe anaitumia, kutuma na kupokea,
Karani hatoachia, kaziye kumfanzia,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Facebook kaingia, na jamvini hutulia,
Hoja zake anatoa, na wenzi kujisomea,
Dunia anaijua, na dunia yamjua,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Twitter aitumia, ofisini akikaa,
Na nyumbani kanunua, iPhone anaijua,
Na mitandao ajua, ndio itatukomboa,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Operesheni ajua, kiendeshi hutumiwa,
Asili anaijua, na bei aitambua,
Vifaa wakinunua, hawawezi tuibia,
Chagueni cha sitini, kabla kitasinzia !

Umuhimu aujua, viwanda kujiwekea,
Mitambo kufyatua, bila nje kununua,
Zana bora maridhawa, vyema kujitengenezea,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

Kunyonya atakataa, kwa Obama na Mamaa,
Kiswahili kuinua, kote tukakitumia,
Na nchi kijijengea, siri ikajiwekea,
Chagueni cha sitini, kablaatasinzia !

No comments: