Sunday, October 7, 2012

Upumbavu una mwisho



Kila jambo na doria, na mipaka yake pia,
Vingine haitokuwa, kuvuka bila ridhaa,
Na wajinga wakijua, mweerevu husinyaa,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Raia wakizijua, zako kumbe ni hadaa,
Heshima watakuvua, kisha uchi kubakia,
Na wengine kuambaa, mbali wakajipitia,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Katika hii dunia, wongo ni tusi libaya,
Ujinga ukatumia, vya wengine kujilia,
Wao wakiligundua, milele hukuchukia,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Macho waklishafungua, kitu hutowaambia,
Wakae na kusikia, bila kuona nazaa,
Hata bora lilokuwa, nalo pia hupindua,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Ajali ukiizua, husemwa ya kujitakia,
Jeruhi na majeraha, mwana wako ndio kuwa,
Ikahofiwa sanaa, na shere za kuzibua,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Sifa hukashifiwa, na jina kudharauliwa,
Heshima itaishia, kisimani kusojaa,
Na busara ukatua, mizigo ilipokaa,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Hatujakuhesabia,  vitabuni kuingia,
Kushoto pia kulia, na ulichozawadiwa,
Hutisha nakuambia, roho unapotolewa,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Hulia wasiolia, na kuhofu mashujaa,
Kikubwa kidogo huwa, tena bado kikapwaya,
Wazima wakazimia, na mafuu kujitambua,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Ni amri maridhawa, wengi wanaitambua,
Ila sasa wachezea, naye awavumilia,
Jinai inshakuwa, wangoja kuhukumiwa,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

Ni vigumu nakwambia, nafasi kujipatia,
Tawba wakaitoa, na huruma kugaiwa,
Bado watang'ang'ania, hadi siku kufikia,
Upumbavu una mwisho, siku ikipambazuka!

No comments: