Wednesday, October 31, 2012

Enzini wanaomwenzi

Msigeuke viazi, mbio kuota mizizi,
Ya wengine kuwa ngozi, nyie mkajidarizi,
Ya chini ikawa dozi, ya juu hamyawezi,
Enzini wanaomwenzi, mtakikwepa kitanzi !

Wenye fedha msienzi, katu hao si wajenzi,
Ni watu wa kujienzi, wepesi wa matanuzi,
Wanafanza uigizi, walipiwe matumizi,
Enzini wanaomwenzi, mtakikwepa kitanzi !

Ni wa rushwa waamuzi, mechi nyingi hawawezi,
Vya umma ni wadowezi, ila wakataa wizi,
Fahari ni yao njozi, na yote yaso azizi,
Enzini wanaomwenzi, mtakikwepa kitanzi !

Enzini wenye mapenzi, na umma kuhafidhi,
Ambao lao zoezi, ni jamii mapinduzi,
Wenyewe wasojienzi, ila fakiri waenzi,
Enzini wanaomwenzi, mtakikwepa kitanzi !

Hili lataka teuzi, na mazuri maamuzi,
Kukataa uenenezi, na ushauri wa juzi,
Eti kuachia ngazi, aipate mwanagenzi ?
Enzini wanaomwenzi, mtakikwepa kitanzi !

Wasitudhani machizi, au teja wapuuzi,
Wakayaona machozi,  imetuzidia dozi,
Nawaapia bazazi, ya kwao yote ni wazi,
Enzini wanaomwenzi, mtakikwepa kitanzi !

Si wa jana ni wa juzi, twalitoa pingamizi,
Watu wengine maradhi, nchi ikipata kazi,
Hufa kwacho kikohozi, cha uroho na uwizi,
Enzini wanaomwenzi, mtakikwepa kitanzi !

No comments: