Sunday, October 7, 2012

Kauli za mnafiki



Mwenyewe humgeukia, kauli za mnafiki,
Kweli anapopindua, na kuitia hamaki,
Watu wakamgundua, siye aliye na haki,
Kauli za mnafiki, mwenyewe humgeukia.

Ukweli humkimbia, akawa haeleweki,
Mantiki ikavia, na hoja hazitambuliki,
Wakamnyanyapaa, aombao urafiki,
Kauli za mnafiki, mwenyewe humgeukia.

Hata wake humwambaa, wakaikosa ashiki,
Ila kama amejaa, watamlia malaki,
Na akisha kuishiwa, tena huwa hatamaniki,
Kauli za mnafiki, mwenyewe humgeukia.

Sio wa kujitambua, hajijui mnafiki,
Ila hufata tamaa, la kweli haambiliki,
Mchana si asubuhi, huja akataharuki,
Kauli za mnafiki, mwenyewe humgeukia.

Vyote huja kupotea, ikawa siyo riziki,
Heshima ikatitia, akabaki hapendeki,
Na rafiki hukimbia, waliomlia lukuki,
Kauli za mnafiki, mwenyewe humgeukia.



No comments: