Tuesday, October 16, 2012

Majoho si utukufu



Ukubwa si utukufu, waweza kuwa uhuni,
Na ndani kuna mikufu, ya hadaa na zaini,
Wako wengi maarufu, lakini kwa uhayawani,
Majoho si utukufu, kuna mengine hadaa!

Kuna mengine tarafu, kaibariki shetani,
Wakajitia shaufu, kuenziwa hadharani,
Lakini kwenye mabafu, wanaiziua imani,
Majoho si utukufu, kuna mengine hadaa!

Wanayaenzi machafu, hayo ndiyo madhumuni,
Katika yao madafu, hakunao ulaini,
Wasakao umaarufu, wautaka kuzaini,
Majoho si utukufu, kuna mengine hadaa!

Moyoni wana maghofu, ya haramu na shetani,
Hawanao uongofu, ila ni umajinuni,
Wadhani wana marefu, kumbe yafa ukingoni,
Majoho si utukufu, kuna mengine hadaa!

Hakika wa utukufu, huuoni duniani,
Twajaliwa udhaifu, na kujifanya yakini,
Tungelihoji maoni, mzuri haonekani,
Majoho si utukufu, kuna mengine hadaa!

Wataka yao sadifu, hata ya kimuumiani,
Wajitie wakunjufu, watu wakawazaini,
Yao yakishawakifu, mirija wakabaini,
Majoho si utukufu, kuna mengine hadaa!

Taifa likadhoofu, watu wakose amani,
Wachukiwe maarufu, kinyaa wawe kundini,
Ikawa mintaarafu, ni adawa kitalini,
Majoho si utukufu, kuna mengine hadaa!

Mwaisusa misahafu, haya mngelibaini,
Si ya jana ni arifu, yameanzia zamani,
Sasa mjitaarifu, mkarejea imani,
Majoho si utukufu, kuna mengine hadaa!


No comments: