Tuesday, October 16, 2012

Nimealikwa karamu

WAMEZUKA chakaramu, mbinu wanazifahamu,
Wanialika karamu, sijui kinachogharimu,
Sio mimi ni kaumu, yatakiwa kujihimu,
Nimealikwa karamu, kula nyumba na magari !

Mualiko ni muhimu, ikulu wameshaazimu,
Na mimi sijifahamu, hivyo hivyo naazimu,
Ingawa huko kuzimu, nahisi wanalaumu,
Nimealikwa karamu, kula nyumba na magari !

Fikra hizi zidumu, au jama zisidumu ?
Vitu visivyo na damu, kuwa mlo wa karamu,
Kijani wamejihimu, mwilini wameazimu,
Nimealikwa karamu, kula nyumba na magari !

Kijani wameazimu, mwilini kwenda kaimu,
Na humo kwenye karamu, kitakuwa ni adimu,
Najiona mwenda wazimu, kukubali  ukarimu,
Nimealikwa karamu, kula nyumba na magari !

Tano sintowadhulumu, unatosha ukarimu,
Ninaiacha beramu, kutafakari salamu,
Mshumaa mashamushamu, waizimia kaumu?
Nimealikwa karamu, kula nyumba na magari !

Anayemanya Alamu, kwa hili kutogharimu,
Ila naiona haramu, yaathirika kaumu,
Njaa inatakadamu, pasina la kurehemu,
Nimealikwa karamu, kula nyumba na magari !

No comments: