Wednesday, October 31, 2012

Uombeayo wengine



WENZAKO waliokuwa, wawaombea ubaya,
Siachi kukushangaa, na uzima kuhofia,
Manani kalikataa, niyo ni husda mbaya,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Uganga sijaupewa, ya keshosijayajua,
Mtabiri haijawa, dhalili mimi nikawa,
Ila nikiangalia, yapo ya kuashiria,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Kwa kuotesha ubaya, mbegu huwa zachipua,
Na mimea ikikua, huwezi tunga kuzaa,
Si zuri linalokuwa, linanitia kinaya,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Gizani tulipokuwa, hili halikuzagaa,
Ila toka kuingia, tivii sasalasambaa,
Watu wakiangaziwa, kuropoka ni tabia,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Nuruni wajishushua, kutamka lisofaa,
Akili wakidhania, hapo wameitumia,
Na pointi imeingia, goli wamejifungia,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Kumbe wazua nazaa, tendo likawachukia,
Ulimi kujililia, adhabu kuihofia,
Na moyo ukasinyaa, kwa huruma kuingiwa,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Kiumbe ukijaliwa, nakuasa nyenyekea,
Udogo ukajitia, na dhaifu  kuridhia,
Huna unalolijua, Mola pekee ajua,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Ya kesho yana tabia, vingine yakatokea,
Vile ulivyodhania, kinyume chake yakawa,
Hiyo aibu na haya, hapo utaikimbia ?
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Mabaya kuwaombea, wenzio wanaojaliwa,
Hayawezi saidia, yako mazuri yakwa,
Zaidi hushindiliwa, chini ukadidimia,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Ila kama hiyo dua, kulaani yakubaliwa,
Ubaya ukitendewa, lazima mja kulia,
Pengine watakusikia, shimoni wakakutoa,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Yusufu yalimtokea, nduguze kumfanzia,
Baya hakuwaombea, ila kaiomba dua,
Mwenyezi kumuokoa, kwa yoyote ile njia,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Utumwani kanunuliwa, huko kazidi kung'aa,
Na ukuu akapewa, wizara kusimamia,
Kaenzi walozaliwa, hata kuja wasaidia,
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

Na wewe ungelikuwa, nini walifikiria,
Si shimoni 'ngewatia, ukaondoa udhia,
Mzaliwa ukamfaa, kwa baba mkarejea?
Uombeyao wengine, yasije kupata wewe !

No comments: