Sunday, October 7, 2012

Ufalme jadi yao



Kazi kufa mazoea, ila kwa choyo na hadaa,
Usultani kuvia, hivi nani kakwambia,
Bado unaendelea, na wengi waulilia,
Ufalme jadi yao, viongozi Afrika!

Udhiaifu tumejaa, viumbe kwenye dunia,
Ngozi tunaivutia, ngoma kuiwambia,
Pale tulipokaa, na wengine kuwazoa,
Ufalme jadi yao, viongozi Afrika!

Na kila anayezaa, chake hukiangalia,
Bila ya kujitambua, mitihani ilokuwa,
Mapenzi yakaishia, sumu ya kutuondoa,
Ufalme jadi yao, viongozi Afrika!

Tume mngeangalia, jinsi ya kuyazuia,
Rohoni yaliyojaa, wazi tusiyoambiwa,
Dira kutotupotea, kwingine kuelekea,
Ufalme jadi yao, viongozi Afrika!

Mifumo kuifumua, ubaguzi kuongoa,
Na uchama kuua, huru wananchi wakawa,
Kasumba  kuiondoa, upinzani kuenea,
Ufalme jadi yao, viongozi Afrika!

Hili sote latufaa, mtawala na mtawaliwa,
Afya pia nayo siha, mwilini ikatujaa,
Na uoza  kuondoa, bora tukayachagua,
Ufalme jadi yao, viongozi Afrika!

Mizani kuangalia, sawa kuwa tasnia,
Na siasa kutegea, chini kuiangushia,
Kila anayekimbilia, kujua ajitolea,
Ufalme jadi yao, viongozi Afrika!

Ujira ukiondoa, wengi wataukimbia,
Na muundo kutanzua, uwazi utaingia,
Kila mwenye kudandia, nauli kwenda kutoa,
Ufalme jadi yao, viongozi Afrika!

No comments: