Sunday, October 7, 2012

Kimya mpenzi wangu

Nampenda Ukimya, kwa tabia na mapozi,
Kwa hakika katulia, si mtu wa maongezi,
Ila langu alijua, sihitaji usakizi,
Kimya mpenzi wangu, ni nani zaidi yake ?

Hata bila kuongea, mie kwake niko wazi,
Nina raha aijua, kwenye dhiki mdowezi,
Na siku haitoishia, asiwe ni mng'amuzi,
Kimya mpenzi wangu, ni nani zaidi yake ?

Nampenda kwa tabia, pia yake maamuzi,
Kati akiingilia, hakuna wa kuniudhi,
Huwa ninajiondoa, ukabakia ushuzi,
Kimya mpenzi wangu, ni nani zaidi yake ?

Nampenda Ukimya, pawapo na wapuuzi,
Masikio humwatia, akasikiza ajizi,
Naye akaniambia, nimtukuze Mwenyezi,
Kimya mpenzi wangu, ni nani zaidi yake ?

Kumtaja hufurahia, hunikumbusha Azizi,
Na kila akiingia, akanipa mazoezi,
Tasbihi kuzitwaa, kumtukuza Muizzi,
Kimya mpenzi wangu, ni nani zaidi yake ?

Nimemkubali Ukimya, na kuipanda mizizi,
Hapa kwake natulia, ngoma hii kwangu saizi,
Wengine ninakimbia, kelele zao siwezi,
Kimya mpenzi wangu, ni nani zaidi yake ?

Anitosha kadiria, hanichoshi, hanikwazi,
Kila nikimhitajia, wala hafanyi ajizi,
Huja nami katulia, nikapata usingizi,
Kimya mpenzi wangu, ni nani zaidi yake ?

Pendo nimetamkiwa,  kuliachia siwezi,
Yabidi kushikilia, kwa miaka ni mjuzi,
Nalo nikipalilia, nyasi kutoa si kazi,
Kimya mpenzi wangu, ni nani zaidi yake ?

No comments: