Sunday, October 7, 2012

Taifa pasi na baba



Wakambo wamekataa, pembeni wajikalia,
Na nchi waangalia, kama fumbo lilokuwa,
Mradi wanajilia, chao basi watulia,
Taifa pasi na baba, uyatima unatisha!

Baba ametukimbia, na wadogo wajitoa,
Mzigo wajionea, kimo yamewazidia,
Arijojo tunapaa, portangi  laishiliia,
Taifa pasi na baba, uyatima unatisha!

Nyumbani watuondoa, wageni kuwaachia,
Na mali wazichukua, zetu zao zinakuwa,
Walezi wanaotulea, kidogo wakigaiwa,
Taifa pasi na baba, uyatima unatisha!

Walezi wanaotulea, kidogo wakigaiwa,
Kimya wakiswalia, na dua za kujililia,
Wanyonge kusahauliwa, kadari ikaachiwa,
Taifa pasi na baba, uyatima unatisha!

Kamba kwao wavutia, wao, ndugu na jamaa,
Binafsi vilivyokua, wao tu wawachukua,
Mayatima watambaa, wanashindwa kutembea,
Taifa pasi na baba, uyatima unatisha!

Mikono wainyanyua, yao mema kujaliwa,
Hapo wakikumbukia, mtume aliyekimbia,
Watu akawaachia, zahama kuwafikia,
Taifa basi na baba, uyatima unatisha!

Watu akawaachia, zahama kuwafikia,
Aliishi kijamaa, wao kuona kinyamyua,
Wamekuwa wanyanyua,  musuli wanafyatua,
Taifa basi na baba, uyatima unatisha!

Maguvu wanatumia, yao kulazimishiwa,
Wakazipinda sheria, na haki kuzibomoa,
Lao lazima likawa, mazuri au mabaya,
Taifa basi na baba, uyatima unatisha!




No comments: