Sunday, October 7, 2012

Bepari kawa mjamaa



Uhayawani huzua, nyang'au watu wakawa,
Ndicho kinachotokea, masikini Tanzania,
Aibu zinatupaa, kwa mali kuzililia,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Juzi na jana tulikuwa, twaamini ujamaa,
Kiongozi kujaliwa, makuu asiyekuwa,
Leo tulichojaliwa, Mola ndio anajua,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Mbio nje twafulia, Olympiki zinapokuwa,
Ila hizi za magunia, fedha kujilimbikizia,
Kila mmoja ajua, hata kutaka kuua,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Tunajaza magunia, na Uswizi kuchukua,
Taifa kulipakua, wengine kwanda kuwafaa,
Masikini kubakia, ombaomba tulokuwa,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Fahari twashangilia, na iktisadi kuvia,
Nchi ya wanaotumbua, kila hali kutanua,
Hali wengi wanalia, aina kila ukiwa,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Mwenye shibe kavimbiwa, hamjui mwenye njaa,
Mkate ukililia, kula keki, hukwambia,
Mhoga haujaujua, tena kwa siku kadhaa,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Wale wanaoishiwa, kwa majukumu  kuzidia,
Huwa wanaambiwa, ujinga wamejitakia,
Eti wasingelizaa, maisha bora yangekuwa,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Uhalali wajitia, vyao wamejichumia,
Jasho lao wametoa, na akili kutumia,
Ila mwalimu najua, ukweli aliujua,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Ila mwalimu najua, ukweli aliujua,
Unyonyaji ukiingia, ndivyo hivyo inakuwa,
Fukara hukaangiwa, vifuta anayotoa,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

Manani wanisikia, na hali yangu wajua,
Lipi la kukuambia, ilaafu kungojea,
Dua kutakabalia, mepesi yangu yakawa,
Leo yanayotokea, mjamaa kuwa bepari!

No comments: