Wednesday, October 31, 2012

Kwanini upate dhambi

MJA mkosa subira, maisha wayachezea,
Yakusumbua harara, shetani kukuingia,
Haraka ukiparura, shida utavumilia,
Kwanini upate dhambi, tamaa ya siku moja ?

Mwendo huo wa hasara, weye uliochukua,
Unakosa maghufira, kila siku kurudia,
Tabaguni hadhira, laiti ungeyajua,
Kwanini upate dhambi, tamaa ya siku moja ?

Yakupoteza  papara, kutotaka kuishiwa,
Waona ni masihara, hauwezi kutulia,
Kufuru unaipara, ya kuja kukuumbua,
Kwanini upate dhambi, tamaa ya siku moja ?

Maisha budi dhamra, na dhiki kuvumilia,
Haramu ikakera, kwa kesho kuihofia,
Ukkifanya ajira, halali inakimbia,
Kwanini upate dhambi, tamaa ya siku moja ?

Halali huja kuzira, mbali nawe kukaa,
Na hiyo ndiyo bishara, pepo imeshapotea,
Duniani ni hasra, na akhera wafulia,
Kwanini upate dhambi, tamaa ya siku moja ?

No comments: