Wednesday, October 31, 2012

Hawachambui nafusi

Za mola zake hidaya, katikati huishia,
Hauwezi kujaliwa, yote ukajipatiya,
Ni dhaifu tulokuwa, kidogo tunapatiwa,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Mpenzi malikupewa, nafusi  yakuambia,
Yataka kujisomea, msingi ukaujua,
Una uzuri ubaya, taa ukimulikia,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Ipo tena njema nia, ubaya ukikusudiwa,
Hata ukiumbuliwa, ktio waweza chimbua,
Kidgo unapopewa, kubali kuvumilia,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Kubali kuvumilia, huku unajinasua,
Kwa chache tu hatua, tajiri waweza kuwa,
Wengi wanapofulia, si budi nawe ukawa,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Huchuma aso na nia, na mwenye nia kufa njaa,
Dunia yake hidaya, mpendwa humgawia,
Lugha anayeiua, asili amalizia,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Thamani asiyejua, la nje hung'ang'ania,
Lake akaliachia, lifaalo kumjengea,
Kiumbe alolaaniwa, mwasisi hawezi kuwa,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Watu wasiojitambua, hapa wanajipitia,
Wakishashusha shahawa, na matumbo kuwajaa,
Zaidi kufikiria, kwao ni pata potea,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

UKiona historia, ni usipopatazamia,
Maombo yanapoanzia, nako yakatunukiwa,
Kukua na kuendelea, na koe yakaenea,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Tajiri alowazaa, fakiri huja jifia,
Na yatima hulelewa, tajiri akaja kuwa,
Na anayeonelewa, mkombozi huja kuwa,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Alotakiwa uawa, huja kukombolewa,
Usultani kutwaa, na milki kujiundia,
Kubwa na inayozagaa, dunia ikamtambua,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Kiswahili nacho pia, hatua itafikia,
Watatokea shujaa, kuja kukipigania,
Cha kwao wakatumia, bila ya kutegemea,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Hila wakazitambua, mkoloni kuzitia,
Lugha yake kutumia, hata isipowafaa,
Mfukoni huwatia, wakubwa akawalea,
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.

Watoto huwatukua, shuleni akawatia,
Mapema inavyokuwa, huko kwake malkia,
Nini utamuambia, yule alofadhiliwa ?
Hawachambui nafusi, somo lao kujifunza.





No comments: