Sunday, October 7, 2012

Ahadi ni kubwa deni



LAITI ningelijua, ahadi nisingetoa,
Mwalimu kaniambia, eti hilo deni huwa,
Sio tu kwenye dunia, akhera lanifatia,
Ahadi ni kubwa deni, duniani na akhera!

Wanangu nimekosea, ahadi hizo kutoa,
Uwezo si kujaliwa, na nguvu zaniishia,
Radhi nawaangukia, lawama kuziondoa,
Ahadi ni kubwa deni, duniani na akhera!

Laiti ningelijua, ishallah ningetoa,
Maana yeye ndo mjua, mbele atangulia,
Mutawakali ni njia, mimi sikumtumia,
Ahadi ni kubwa deni, duniani na akhera!

Pekee nilidhania, naweza jitegemea,
Yote kuwatimizia, nanyi mkafurahia,
Ila njiani najua, safari yaendelea,
Ahadi ni kubwa deni, duniani na akhera!

Pembeni aliyekaa, bado aniangalia,
Sasa namgeukia, kupata yake ridhaa,
Laiti ningelijua, kwanza ningemuendea,
Ahadi ni kubwa deni, duniani na akhera!

Muda haujaishia, nadhani anisikia,
Japo kinya amekaa, udhaifu anijua,
Huruma kunipatia, hasara haitokuwa,
Ahadi ni kubwa deni, duniani na akhera!

Kiumbe sikujijua, ngazi nilitangulia,
Hali si wa kuelewa, njia ya kuifatia,
Na sasa nimegundua, ni kuihama dunia,
Ahadi ni kubwa deni, duniani na akhera!

No comments: