Wednesday, October 31, 2012

Waandishi mkiamua




Kalamu mkiamua, bora itatupatia,
Ila mkinunuliwa, tunaenda kufulia,
Viumbe wenye hadaa, yao wanadhamiria,
Waandishi mkiamua, wahuni watakimbia !

Habarini kuwatia, bora watajidhania,
Kelele wakajitia, uchuzi waliokuwa,
Wao wanshanunuliwa, nanyi wanawanunua ?
Waandishi mkiamua, waja viongozi bora!

Hekima kuitumia, kwa mbele kuangalia,
Hawi asiyetambua, nini atatuibia,
Ikulu kukimbilia, fajiri latoka jua
Waandishi mkiamua, wahuni watakimbia !

Au leseni wapewa, ulinzi kuingilia,
Waliowatangulia, salama kujionea,
Hilo sintolielewa, lazima kufafanuliwa,
Waandishi mkiamua, waja viongozi bora!

Mwatakiwa kuchugua, watu walipoanzia,
Nini kiloamuliwa, na wakakubaliwa,
Sasa yanayotokea, dira ipi yachukua ?
Waandishi mkiamua, wahuni watakimbia !

Marikani kutuoa, Mchina atatwangalia,
Na Irani kumwatia, yake akajifanzia ?
Au Vietnam twawa, miaka inayoingia ?
Waandishi mkiamua, waja viongozi bora!

Vijipesa mkipewa, na vigari kutembelea,
Hivi mnajitambua, na yao mnayaelewa ?
Kipi wanachochukua, hadi wakawaridhia ?
Waandishi mkiamua, wahuni watakimbia !

Palipo na nzuri nia, gharama hapatingia,
Anayekaa kimya, wala mjinga hajawa,
Na kila munuliwa, kaziye ni kutumiwa,
Waandishi mkiamua, waja viongozi bora!

Mwatakiwa kuchagua, bora kitakachotufaa,
Hasara kisotutia, hadi amani kwachia,
Misingi mkililia, watu bora mtakuwa,
Waandishi mkiamua, wahuni watakimbia !

Saburi inatakiwa, si fedha kukimbilia,
Puani hukutokea, kesho ukazijutia,
Wana 'kija kuchinjiwa,na wewe kuhujumiwa,
Waandishi mkiamua, waja viongozi bora!

No comments: