Sunday, October 7, 2012

hananasif



Utu ukiwaishia, mngeuka wanyama!
Mambo mkajifanyia, bila kujali salama,
Roho mkazisumbua, hata vichanga vikiwa,
Halali mkijitia, yawaruhusu sheria!

SikataI kubomoa, kama mlishaamua,
Ila ninacholilia, ni utu ulivyopwaya,
Wanyama watu kuwa, nje wakajilalia,
Akili ikitumiwa, huruma mngeijua!

Red cross kuwatia, watu wakaangalia,
Na mgambo kuchuka, wasije wakaibiwa,
Salama inapokuwa, mengine kutosumbua,
Utu ghali haujawa, maguvu msipotumia!


Serikali ya kujua, jukumu pia kulea,
Kuna wagumu kwelewa, hatua inatakiwa,
Kisomo wakakikipewa, taratibu kuchambua,
Mkajenga kuchukkiwa, hata na wasiochukia!

Watu wengine wakiwa, njaaa imewazidia,
Na wanalofikiria, kuhama haijatokea,
Hungojea kujifia, kwa tegemeo kutwaa,
Maisha katu usawa, wote haitojalia!

Wapo wanaotambua, kwa muda wakaelewa,
Na wengine wachukua, masaa kujitambua,
Mizani ukitumia, wengine utawaua,
Sheria iso huruma, huitwa ni ukatili!

Angalia historia, nanyi wapi mwatokea,
Vijiji tuliwajengea, mkawa mwasaidia,
Leo upofu watia, hata kwa mnayoyajua?
Wenzie asiyejali, ukubwa haumfai!

Wananchi kuwalea, kazi mliyopewa,
Uyatima mkitia, na ukatili kujaa,
Nani kuwageukia, ende huko kuwafaa,
Hata wanaokataa, kulindwa pia sheria!

Kama wana wanakuwa, hao wanaotawaliwa,
Kisa kinachotokea, kwenu ndiko chaanzia,
Ubaba mlijitia, leo mwashindwa kulea?
Na umama mwakataa, japo mnafanania?

Laiti ningelikuwa, mara sabini 'ngetua,
Polepole kuwambia, na mipango kuibua,
Ushirikishi ni njia, mwashindwa kuutumia?
Raia ukimwachia, kwa njaa analemaa!

Hata waliofidiwa, yafaa kuwaongoa,
Mtanzania twamjua, matata alivyokuwa,
Ila sisi twatakiwa, dhaifu kuangalia,
Utu unappungua, nchi huwa yaugua!

Hananasif radhia, kilio nakisikia,
Utu nimeugundua, umeisha Tanzania,
Maguvu tunatumia, hata yasipotakiwa,
Ukiwa ninauchukua, umma kuutangazia!

Atamulika Alaa, mwingi wa kuangalia,
Ni yatima mmekuwa, ndugu zangu Tanzania,
Wao wanaangalia, sio wasiowajua,
Mola atawaangalia, na nusura kuijua!

Mshale nawarushia, moyoni utaingia,
Uvikiuta kujua, jangwani hawakuachiwa,
Misaada walimwaiwa, hadi walipotembea,
Hili si gumu najua, kwa kila anayeelewa!

Poleni Hananasif, kwa kubakia wakiwa,
Huu wetu udhaifu, gharama kwenu ikawa,
Tumezibeba tarafu, na moyo kutu kutia,
Tuendako nahofia, mumiani tutakuwa!

No comments: