Sunday, October 7, 2012

Mnafiki ajijua



Mwenyewe hajiamini, ajabu iliyokuwa,
Ajua yuko shetani, mbele ametangulia,
Kamfanya aamini, bila ya kuaminiwa,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Hujishusha kwa thamani, hata  alilosomea,
Akatua mnadani, kwenda naye kunadiwa,
Bei wakiibaini, ya kwao hupigania,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Huritadi duniani, na pepo kumkimbia,
Dunia anayethamini, hii ndiyo yao njia,
Hugeuka afkani, hadi roho kutwaliwa,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Huiuza yake dini, shilingi ikamnunua,
Akajiona rahani, kumbe moto achochea,
Hakika ni majinuni, laiti angejijua,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Vitabu vinabaini,  makazi waliyopewa,
Kila mkosa imani. pabaya kwenda ingia,
Hufurahi duniani, kwa masaa yalokuwa,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Hufurahi duniani, kwa masaa yalokuwa,
Yeye akawa adhani, ni miaka imekuwa,
Akishtuka mtani, motoni asubiriwa,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Anatupenda Manani, tawba tukiitoa,
Husahau kwa yakini, twaha akatugeea,
Kila mwenye kubaini, hili hulikimbilia,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Hususani muumini, kesho wanaohofia,
Wakijua duniani, si pahala pa kukaa,
Bado wangali njiani, fikio kuelekea,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Nakusoma Rahmani, sura inanipatia,
Na tano hamsini, mengi nisiyoyajua,
Kitabu nakiamini, shaka nashindwa kutia,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!

Hata lake haamini, ataka mumuamini,
Kisigino ni kichwani, na aibu hayawani,
Huyu kiumbe afkani, hadhi duni duniani,
Mnafiki ajijua, mwenyewe hajiamini!


No comments: