Monday, October 15, 2012
V I J A N A L E O T A I F A
LAITI mkiamua, taifa leo vijana,
Hatua mtachukua, uoza kwondokana,
Nchi mkaifagia, kila kitu mkasana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Nchi inawangojea, kutumikia vijana,
Ndani mliochimbiwa, mso kitu cha maana,
Na nje mliokimbia, kuukataa utwana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Hamsini kutumia, sisi sasa si vijana,
Uzee unaingia,twafanana kama jana?
Kwa kuwa tunaachia, nchi inaumizana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Kazi tele zimejaa, tunaiona hiyana,
Ya kwanza yakuanzia, ni nyumba kujengeana,
Vijijini kuingia, kwa hali tukapambana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Wazee wanangojea, sadaka kupatikana,
Vijana ninawajua, Pongwe na Kimanzichana,
Nyenzo mkisaidiwa, nyumba zitaonekana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Na maji nayo pia, yaweza kupatikana,
Akili tukitumia, tukazingeneza zana,
Hizo za kununuliwa, ndizo zinazotubana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Miaka tulofikia, ni ya kutengeza zana,
Zote tunazotumia, maji yatapatikana,
Zoezi likaendelea, bila ya kukwamishana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Hadithi ukisikia, kukwama kupatikana,
Ni zana tumefulia, twangoja zitoke China,
Hali tukijitambua, kuunda yawezekana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Trekta ninajua, kuunda si kazi sana,
Moyo ndio watakiwa, na maono kuyaona,
Ombaomba kuzoea, hiana twafanyiana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Ardhi tutaifukua, tuweze kulima sana,
Chakula kujipatia, na kingine kuuuziana,
Marikani na Asia, nja tukatlizana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Uvuvi tunafulia, hapa pwani tunaona,
Samaki twashindwa vua, kwa udhia na hiana,
Misiri wameamua, jangwani wanapatikana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Misiri sasa wavua, jangwani kuna amana,
Yametuzunguka maziwa, sisi twasimangana,
Bahari twaiambaa, twavua pasipo zana ?
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Yote ukiangalia, uzee ndiyo hiana,
Kwaisha kufikiria, kwabaki kukimbizana,
Urais kufatia, haya, aibu hatuna,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Leo nimedhamiria, watu kuwachamba sana,
Utoto wanatutia, na upofu wa kutoona,
Wanaizuru dunia, hawana wanalovuna?
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Balozi tukiamua, hao wakawa vijana,
Elimu wataivua, na mbinu zenye kufana,
Wazee wajikalia, pipiefu kuivuns,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Balozi tukiachia, wakatawala vijana,
Ujuzi watahukua, kuja jenga mengi sana,
Nchi iwe yakimbia, si maktaimu kufwatana,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Wazee wang'ang'ania, tija wasipoitia,
Tukazidi kutambaa, badala ya kukimbia,
Ni udhia imekuwa, mwishowe unatakiwa,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Vijana ukiwalea, nyumba mnawaachia,
Waweze jisimamia, na hatua kuchukua,
Ya kwale wakiathiriwa, huja nyumba ikavia,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Vijana mmetimia, kwa wingi mmefikia,
Taifa mmeshakua, nchi inawasikia,
Hii ni demokrasia, idadi mshatimia,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Wenyewe mkizubaa, nchi watawaharibia,
Kifuu kitabakia, nazi nayo isokuwa,
Hata dafu maji kuwa, afadhali ingekuwa,
Vijana leo taifa, sio taifa la kesho !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment