Sunday, October 7, 2012

Hatma ya Tanzania



Naamini inafaa, hatma kuirejea,
Tupate kuyaelewa, mwalimu alotwambia,
Kasema bila  nazaa, ukweli akatwambia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Wenzetu wakajitia, ni viziwi walokuwa,
Usafi wakajitia, wengine uchafu kutia,
Kisha wakajifanzia, yalokuwa, yasokuwa,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Mbio wakazikimbia, madawa wametumia,
Mstari kufikia, hakuna aliyejua,
Tume inatawaliwa, huru bado haijawa,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Ulinzi ukitolewa, pande unaegemea,
Nawe ukifikiria, uchawi utagundua,
Yafa demokrasia, au hai yabakia?
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Ilikuwa njema nia, ila inazainiwa,
Nyadhifa wanaopewa, utoto wanatutia,
Kila ukiangalia, wadhani unataniwa,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

UKubwa wanaopewa, wakanyanyasa raia,
Na matusi kuyatoa, watumishi kwangushia,
Ninadhania yafaa,ya kwao kuyafichua,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Nje usafi wajitia, ndani uchafu wajaa,
Cheto tukiwaachia, hata watu wataua,
Na sintoajabia, kama wanshatangulia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Watu wanajichagua, kikundi kukitetea,
Usawa umepotea, na haki yanunuliwa,
Huko tunakoelekea, mzee alikuhofia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Vijiji vinaugua,vyazidi kujikondea,
Ukimwi utadhania, huko umeshavamia,
Sababu utagundua, uchama umezidia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Watu hawajajitambua, kujua la kuwasaidia,
Kale wanaegemea, nayo inawachezea,
Shere inawaangia,miaka ikipotea,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Nyerere kayagusia, sana kazungumzia,
Uchimvi uliokuwa,ikulu kukimbilia,
Malengo wanafukia, hadi wakichaguliwa,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Hivi sasa wajamaa, mabepari wamekua,
Chama tunachokijua, kila hali chajifia,
Igizo limebakia, na bado hawajajua,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Hawa sasa watishia, ovyo ovyo kuchagua,
Hadhi wasiofikia, nchi izidi kupwaya,
Na hofu wanaotia, unyama kutwanzishia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Laiti ninelipewa, nafasi kuwausia,
Watu ningewaambia, chama kutokuchagua,
Ila kumuangalia, yeyote anayefaa,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Ila kumuangalia, yeyote anayefaa,
Hata huru kuchagua, bila chama kuingia,
Lakini asiye doa, na utu amejaliwa,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Vingine ninahofia, mkenge tutaingia,
Wote ninaowasikia, tuhuma zimewajaa,
Msafi sijamjua, wala sijamsikia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Ndio ninawaambia, Hatma kuirudia,
Pengine mtagundua, mlichoshindwa fichua,
Kongamano kuandaa, kurasa kuzipitia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Makundi kuyakataa, majopo kuyatumia,
Wazi kuzungumzia, vigezo vya kutumia,
Kila chama kutakiwa,ndivyo hivyo kwangalia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Salama nawaombea,wenzangu Watanzania,
Nyumbani mnaokaa, bila kujua dunia,
Na ujanja kuuziwa, nchi unaotuulia,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

Ila mida yafikia, hili kuja kuondoa,
Watu wakachaguliwa, kwa sifa za kutonunua,
Uwezo kwa kuujua, na kipaji kujaliwa,
Hatma ya Tanzania, Nyerere aliijua!

No comments: