Monday, October 15, 2012

Enzi za upiga debe




VIJANA wa Tanzania, hivi sasa waamua,

Minyororo kuitoa, wazee kutumikia,

Uhuru kujipatia, na uongozi kutwaa,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Nchi waliochimbua, na dhahabu kuigawa,

Mashimo kutuachia, wala hai kufukiwa,

Wakageuka bidhaa, na nje kununuliwa,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Mikataba kukataa, na upya tukaanzia,

Uroho wasingekuwa, wote wangetunyanyua,

Nafsi kuwatangulia, leo wanajichukia,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Wao walijifikiria, ya nchi wakaachia,

Imani hawakujaa, kesho yetu kwangalia,

Wao na walichozaa, ndicho muhimu kilikuwa,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Ufisadi waujua, huko ulikoanzia,

Mikono yashuhduia, kwavyo vipi kukataa,

Damu unatapakaa, wasema haujaua?

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Nchi wamezichukua, Uswizi kuzitupia,

Eti kimya wanakaa, lengo kulipotezea,

Wajua Watanzania, kumbukumbu hupotea,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Dowans wanawajua, TANESCO kuhujumiwa,

Siku walioyaanzia, unafiki kuutia,

Chama wanapalilia, sikumoja kuwafaa?

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Makampuni bandia, kazi yao ilikuwa,

Na mikataba kutia, uoza iliyokuwa,

Na wengine kutwambia, wataangusha mvua,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Mungu wakamchezea, kwa akili kujitia,

Wengi wanawanunua, na wao kununuliwa,

Nchi sokoni yatiwa, mchuuzi anangojewa,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Ndio ninawashtua, vijana kujizindua

Wazee mkiachia, vitani watawatia,

Roho zimekua mbaya, ukubwa kuulilia,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Umungu wanajitia, wana kuwalimbikia,

Na vyeo kuwaptia, kina kilichozidia,

Mwalimu angeyajua, nchi asingewaachia,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Maneno mengi watia, kumbukumbu isokuwa,

Machozi wanayotoa, ya mamba wamejaliwa,

Rohoni washangilia, kaondoka mjamaa,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Ubaya wanafukua, na mema kuyachimbia,

Mazuri wakidhania, yeye alishayajua,

Hugeuka ni ubaya, Dracula wa kuua,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Vijana wa Tanzania, wito kwenu nautoa,

Marufuku kutumiwa, watu debe kupigia,

Mwenzenu ni kuchagua, wa rika mliokuwa,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Mwenzenu ni kuchagua, wa rika aliyekuwa,

Mkaanza muandaa, nchi kuja ichukua,

Wakati umeshawadia, taifa kutopotea,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Ni haki kuwaondoa, wazee wasiofaa,

Ulafi waliojaa, uchu na kubwa tamaa,

Isiyoshibika njaa, sikuzote wanalia,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Vyamani wanunuliwa, mfukoni wanatiwa,

Takataka wamekua, rahisi nchi kutoa,

Wageni kuwauzia, mkabaki mnalia,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Wakati umewadia, miezi ya kuamua,

Rushwa mliopokea, kwenda kuishtakia,

Na waliochaguliwa, ngazi wakaziachia,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



Na kisha mkachagua, vijana kwenda gombea,

Rushwa mkiikataa, na usafi kuchagua,

Itaamka Tanzania, vijana kuwashangilia,

Enzi za upiga debe, hatima imefikia.



No comments: