Sunday, October 7, 2012

Vijana tahadharini


Kwa zao kubwa tamaa, nafasi wapigania,
Sio watu kuwafaa, ila wao kujifaa,
Uchu wanaunukia, na denda wanalitoa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Watu hawa radhi huwa, hata kuua jamaa,
Ili wakajipatia, wanachokikimbilia,
Hata kama wanapwaya, kufaa hawajanuia,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Nyie watawatumia, kitu msiotambua,
Mkadhani mwachagua, kumbe mmechaguli\wa,
Kambini kwenda kutiwa, na kisha mkatumiwa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Upofu watawatia, uzuri mkawadhania,
Mkawa mwawapigania, wajao kuwamalizia,
Hali wao wajilia, wanao na pia jamaa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Mwatakiwa fikiria, ukweli mkaujua,
Ndani na nje chungua, kama kweli ana nia,
Nchi kuitumikia, au yeye kujifaa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Ufalme waulilia, mkoloni waliyemtoa,
Sio siri twawajua, wadhani kwalo wazaliwa,
Kuwa wao ndio wafaa, wengine wawakataa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Weneyewe wajichagua, kila safu Tanzania,
Pembeni mkatupiwa, kama si Watanzania,
Hili mkishalijua, wa kumfata mtajua,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Msije nyasi makwa, na ng'ombe kwenda liwa,
Tena hamtobakia, na kesho yenu kujua,
Angalia adilia, uchamungu walopewa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, asiye na historia,
Ya uchama kugandia, ya kwenu kutoyajua,
Ahadi wanaotoa, wakashindwa kulipia,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, alokuwa damu mpya,
Ukale kuuachia, tupate kizazi kipya,
Hatamu kitakachokataa, na halali kuchagua,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, mchumi wa kuchimbua,
Hivyo vinavyopotea, hazina akavitia,
Wala si wa kutumiwa, dhahabu atuibia,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, umeneja wa kujua,
Mambo akatupangia, chanya yanayotakiwa,
Na sio nyingi ruia, dunia zisizofaa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, nje wasiyemnunua,
Sumu akaja chimbua, watu wetu kuwaua,
Na miradi kufungua, mazingira isofaa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, ukabila asokuwa,
Wao akisadia, wengine kutokuwafaa,
Kujuana na kujua, ni cheo chenye kinaya,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, udini asiyejaa,
Dini yake kuifaa, na wengine kusinyaa,
Nchi huja kuigawa, vitani mkaingia,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, waandishi asonunua,
Na redio kuitumia, yake kutangazia,
Na tivii kumtoa, hata kwa lisilotufaa,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, kisasi asiyetia,
Watu akawakomoa, na ulemavu kutia,
Nusura si wa kujua, lao wanakimbilia,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, asiyejilimbikia,
Mali akafikiria, badala ya kujitolea,
Tumbo litatangua, akili zikafatia,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!

Kiongozi atakiwa, ubia anayehofia,
Wa nje kumtumia, nchi wakainunua,
Watumwa tukajakuwa, hapa kwetu Tanzania,
Vijana mkinunuliwa, wenyewe mtauana!


No comments: