Tuesday, October 16, 2012

Kila mvaa kikoi



Utakuwa ni mafuu, kiumbe hujitambui,
Watu ukiwadharau, nao wangali ni hai,
Humjui wa nafuu, wakati ungali hai,
Mja usimdharau, kila mvaa kikoi!

Maisha sumu dharau,  kwa wengine haifai,
Hata ukipanda juu, ya chini huyakimbii,
Hata na wapanda nguu, kileleni hukinai,
Mja usimdharau, kila mvaa kikoi!

Majuto ni mjukuu, asiyesikia rai,
Usitafune tambuu, kwa mate kutujeruhi,
Huonekana bahau, na njia hautambui,
Mja usimdharau, kila mvaa kikoi!

Pumzi zetu kuukuu, tambaa la kukinai,
Mlima si kichuguu, japo wengi hawajui,
Hali sio dafrau, kuchagua hatujui,
Mja usimdharau, kila mvaa kikoi!

Wepesi wa kusahau, viumbe dunia hii,
Na haraka wa malau, hali neno hawajui,
Sambusa si kaukau, havilingani kwa bei,
Mja usimdharau, kila mvaa kikoi!

Ninaliachia dau, niendako sikujui,
Pepo hizi za nahau, niendapo kusabahi,
Naitafuta nafuu, mwenye nayo simjui,
Mja usimdharau, kila mvaa kikoi!


No comments: