Sunday, October 7, 2012

Uungu wameutwaa



Uungu wameutwaa

MJADALA wanazua, na vijembe kuvitia,
Shetani kawazuzua, juu wanavyopepea,
Na sawa wanapaniwa, kama vimungu  wakawa,
Uungu wameutwaa, riziki kunipangia!

Uungu wameutwaa, riziki kunipangia!

Hupanga wakapangua, kila kitu wakijua,
Wakaiweka na nia, riziki kuizuia,
Mja kumuharibia, ya kwake kutotimia,
Uungu wameutwaa, riziki kunipangia!

Na mpaji anajua, moyoni yaliyokuwa,
Yeye awazawadia, hiyana wanailea,
Wahaka waliojaa, shukrani wasokuwa,
Uungu wameutwaa, riziki kunipangia!

Uungu wagombania, ili watu kuumia,
Dhiki wakaziibua, ikaungua dunia,
Wao wakijichumia, kivulini kujilia,
Uungu wameutwaa, riziki kunipangia!

Moyoni nimeridhia, kupata nisilopewa,
Maua kujichumia, maumbile yakizaa,
Na jua kufurahia, kama ilivyo kwa mvua,
Uungu wameutwaa, riziki kunipangia!

Saba ikishatimia, kwa dua kumaliizia,
Rabi kuturahisishia, ngwee iliyobakia,
Huku twamkurubia, na peponi kuingia,
Uungu wameutwaa, riziki kunipangia!

No comments: