Saturday, October 20, 2012

S A D I K I






Sadiki yupo muumba, wa hii yetu dunia,

Viumbe ametuumba, yeye kututangulia,

Na ni kujitia kamba, kingine kuabudia,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki umekosea, na deni unadaiwa,

Hio ulichoamua, wala sawa haikuwa,

Mizani imefulia, uongo inakwambia,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki hujitambui, nafsi yakuchezea,

Na ulicho haujijui, kingine wakidhania,

Kila kukichwa matlai, washindwa kujitambua,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki wewe hujui, maho utayafungua,

Ukaitafuta rai, na ushauri kupewa,

Hakika ukijidai, utazidi kupotea,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki katika haki, utazika unafiki,

Usiwe ni mamluki, nafsi kutobariki,

Dhulumati hapendeki, malaika humshtaki,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki kwenye adili, hulka pasi mushkeli,

Ukaijua akili, ni chanzo cha ujahili,

Na pasinaye Adili, wewe kiumbe dhalili,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki bila ukweli, hubaki kiwiliwili,

Roho ikose fasili, ukianza udahili,

Makabiri zurtumuli, hudhihiri tu ukweli,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki huna imani, unaishi kwa rehani,

Yakini ni upofuni, uishio mskani,

Ukazungukwa na duni, wazidi kuvuta chini,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki ni meli wawa, na dira haukipewa,

Gizani umetokea, na gizani waelekea,

Na wanaokufuatia, lazima watapotea,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki hauelewi, moyo utafunguloiwa,

Nuru kwako haitui. pengine yaegemea,

Ni mapema asubuhi, nafsi unshapewa,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki kweli waua, ili yako kutimia,

Ujinga waununua, roho ukajiuzia,

Laiti ungelijua, katu haitatangulia,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki uongo dawa, vidonge unatumia,

Na teja umeshakua, bilavyo unaugua,

Upatacho hutumia, hata haramu kikiwa,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki umepgawa, ruhani akuchezea,

Maduguli kuibua, kichwani tukamtoa,

Mwenyewe ukijujua, uhuru utaujua,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki unapangua, cha kwako kukibomoa,

Na wanaokusaidia, si wazuri ni wabaya,

Wewe umeng'ang'ania, kama ndugu wamekuwa,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki huna kanuni, ovyo unajipitia,

Hautopata auni, bila kuacha udhia,

Unavaaje gauni, mwanamke hujakuwa,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki huna ratiba, mengi kwako ni kadhaba,

Imani yako haba, haitojaza kibaba,

Na huu kwetu msiba, twamgeukia Toba,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki una hamaki, kama mkizi samaki,

Na hauitaki iliki, mhemuko isolaki,

Kikulacho kikibaki, hapabakii rafiki,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki una kisasi, alicholaani Qudusi,

Kinacholea nuksi, kwa uchache wa durusi,

Iangale nafusi, maisha yana mikasi,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki sio bidhaa, kiumbe kununuliwa,

Kama ulikuwa ujuha, sasa kwanzia kataa,

Mola ukimrudia, haachi kukuangalia,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki yafa hekima, yafaa kuifufua,

Pasiyo kuna zahama, huizamisha dunia,

Na za kupikwa tuhuma, mwenyewe ukajiumbua,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki tupu busara, tupu labaki gunia,

Na duara walitia, kitu kisichotambua,

Unavyo visivyochanua, wala haviwi maua,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki unapotea, na hiyo si yako njia,

Kinyume unapitia, wenda kwingine tokea,

Na ukija uliziwa, uliko hawatajua,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki katika watu, usijifanye ni jitu,

Hatamki mtu kitu, yakawa ni kisu butu,

Kila analothubutu, huwa hachezi upatu,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



Sadiki katika dua, Mola atakuafua,

Dhuluma anayejaliwa, na wake hudhulumiwa,

Na siku ikifikia, aibu huiogea,

Sadiki uyaamini, mtu bora utakuwa!



No comments: